Kampuni ya God Mark
Funeral Director inayotoa huduma za mazishi mjini Moshi, imetoa punguzo
la asilimia 30 kwa mtu atakayenunua jeneza akiwa hai.
Mkurugenzi wa kampuni
hiyo Macmillan Siraki alisema kuwa, kununua jeneza mtu akiwa hai
haisababishi nuksi au balaa lolote kama baadhi ya watu wanavyodhani.
“Sisi kazi yetu ni kusaidia kuwapeleka mbinguni watu waliojiandaa vyema
kwa kukaa karibu na Mungu wao. Tumeona tutoe punguzo mtu akinunua jeneza
akiwa mzima,” alisema.
Siraki alisema bei ya
majeneza yanayouzwa na kampuni hiyo ni kati ya shilingi 300,000 na
650,000 kulingana na ubora. Punguzo la asilimia 30 ni kati ya shilingi
90,000 na 195,000.
“Unajua ukishakufa hujui
hata aina ya jeneza ulilozikwa nalo, lakini wapo wanaopenda wachague
linalolingana na hadhi yake – hao ndio hasa tunaowalenga. Siyo jambo
baya hata kidogo,” alisema.
Mchungaji wa Kanisa la
Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini, Samwel
Msack alisema suala hilo ni zuri na mtu akinunua jeneza lake haina maana
atakufa mapema. “Hata kwenye Biblia, Abraham – baba wa imani, alinunua
shamba la kuzikiwa yeye, familia yake na ndugu zake kiasi cha kwa 400
kutoka kwa mtu anaitwa Banheth, mbona hakufa hapo hapo?” alihoji.
Wakili wa kujitegemea,
Albert Msando alisema kwa utamaduni wa Watanzania, suala hilo linaweza
kuwa gumu kwa sababu ya dhana ya watu kuogopa kifo. Alisema jambo hilo
halina tofauti na kuandika wosia ambao kuna dhana imejengeka kuwa mtu
akiandika atakufa haraka wakati ukweli ni kuwa hauna uhusiano na siku
yako ya kifo.
HT: Mwananchi.
0 comments :
Post a Comment