Serikali
ya Tanzania na kampuni za ujenzi za Uturuki na Ureno, zimesaini mkataba
wa ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha kimataifa (standard gauge)
kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro wenye thamani ya dola za Marekani
bilioni 1.21 (Sh trilioni 2.66).
Kati ya fedha hizo, dola za Marekani bilioni 1.21 (Sh trilioni 2.2) ndiyo gharama halisi ya ujenzi wa kipande hicho na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ni dola milioni 1.85 (Sh bilioni 406).
Mradi
huo unaotarajiwa kukamilika ndani ya miaka miwili na nusu, utaifanya
Tanzania kuwa nchi ya pili barani Afrika yenye reli kama hiyo ambayo
inaweza kupitisha treni ya umeme inayotembea kwa mwendo wa kasi.
Akizungumza
kabla ya kutilia saini mkataba huo jana, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, alisema kwa sasa barani Afrika,
Morocco ndiyo yenye reli kama hiyo inayopitisha treni inayotembea kasi
ya kilomita 200 kwa saa.
Kukamilika
kwa kipande cha reli ya Dar es Salaam mpaka Morogoro, treni inayotembea
kwa kasi ya kilomita 160 kwa saa itaweza kupita.
Profesa Mbarawa alisema hali hiyo itafanya safari ya kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro kuwa saa 1:30.
Kukamilika
kwa awamu ya pili ya reli hiyo kutoka Morogoro mpaka Dodoma kutaifanya
safari ya treni hiyo ya umeme kutoka Dar es Salaam kwenda makao makuu ya
nchi kwa kutumia saa 2:30 huku kitakapomalizika kipande cha Dar es
Salaam mpaka Mwanza, kutaifanya treni hiyo kusafiri kutoka Dar es Salaam
mpaka mkoa huo wa Kanda ya Ziwa kwa saa 7:30.
Kampuni
zilizotia saini ujenzi wa reli hiyo ni Yapi Merkenzi Instant Ve Sanayi
A.S ya Uturuki ambayo imeungana na Mota-Engil, Engenharia E and
Construcao S.A ya Ureno.
Awamu
ya kwanza ya reli hiyo kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro itakuwa na
urefu wa kilomita 300 kati yake kilomita 205 ni njia kuu na 95 ni njia
za kupishania treni.
Ujenzi huo utahusisha pia uzio wa usalama kutokana na reli hiyo kutumia umeme pamoja na ujenzi wa vivuko kwa watu na wanyama.
Profesa Mbarawa alisema:
“Wakati tunafikiria ujenzi wa reli hii tuliwatuma vijana Kenya,
Ethiopia na Nigeria kuangalia namna ambavyo wenzetu wamefanikiwa,
tulilenga kuepuka makosa ambayo wenzetu waliyafanya ili tusiyarudie.
“Tuligundua
nchi hizi treni yao inakwenda kilomita 120 kwa saa, tukajiuliza kwanini
tusipate inayokwenda 160? Sasa tumepata inayokwenda kasi zaidi. Ya
Kenya na Nigeria zinatumia mafuta, tukaenda Ethiopia tukakuta wao
wanatumia umeme, tukaona kwanini na sisi tusije na inayotumia umeme?
Sasa tumefanikiwa.”
Alisema
reli hiyo itakuwa na uwezo wa kubeba mzigo wa tani 35 kwa excel moja,
ikilinganishwa na sasa ambapo reli ya zamani (meter gauge) ina uwezo wa
kubeba tani 14 kwa excel moja.
Reli
hiyo itakuwa na uwezo wa kusafirisha tani milioni 17 za mizigo kwa
mwaka kutoka tani milioni tano za sasa, hivyo kuifanya kuwa daraja la
uchumi wa nchi kwa kuiunganisha na nchi za jirani ambazo hazina bandari.
“Tumeamua
kufanya mradi huu kwa kasi na kuzingatia kiwango cha ubora wa reli
yenyewe lakini pia gharama za ujenzi. Usafiri wa reli ni nafuu na
inabeba mizigo mingi,” alisema Profesa Mbarawa.
Alisema
itakapokamilika reli hiyo, itarahisisha usafiri ambapo mtu anaweza
kuishi Dodoma au Morogoro na akafanya kazi Dar es Salaam.
Alisema
gharama ya ujenzi huo inategemewa kushuka kwa eneo la kuanzia Morogoro
hadi Mwanza kwani eneo hilo si la mwinuko kama ilivyo kutoka Dar es
Salaam mpaka Morogoro.
Aliongeza
kuwa katika mwaka huu wa fedha 2016/2017, Serikali itaongeza fedha za
ujenzi wa reli hiyo ikiwa ni pamoja na kuomba mikopo kutoka kwa wahisani
ili kuhakikisha wanaiunganisha Tanzania na kuifanya kuwa karibu zaidi
tofauti na ilivyo sasa.
Alisema
jumla ya kampuni 40 ziliomba zabuni ya kujenga reli hiyo lakini YAPI ya
Uturuki inayoshirikiana na Mota ndiyo iliyorudisha zabuni.
Akizungumzia kuhusu kampuni za China kutopewa zabuni ya ujenzi wa reli hiyo alisema ni kwasababu hazikurudisha zabuni zao.
Wakati
huo huo Waziri Mbarawa alisema tayari Serikali imetangaza zabuni ya
ujenzi wa reli hiyo kuanzia Morogoro hadi Makutupora kilomita 336,
Makutupora hadi Tabora 294, Tabora hadi Isaka 133 na Isaka hadi Mwanza
248.
“Tunaikaribisha
kampuni yoyote inayotaka kujenga na hakuna kampuni tutakayoionea ila
uwezo wa kampuni na gharama za ujenzi zitaangaliwa,” alisema Waziri Mbarawa.
Akizungumza
katika utilianaji saini huo Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya
Miundombinu, Profesa Norman King, alisema kuanza kwa ujenzi wa reli hiyo
ni kutimia kwa ndoto za Rais Dk. John Magufuli za kuona Tanzania
inakamilisha ujenzi wa reli ya kiwango cha kimataifa.
“Pamoja
na kuonekana kwa wengi tumechelewa lakini kuchelewa huku ni kuzuri kwa
sababu tumeua ndege wawili kwa jiwe moja kwa kupata treni inayokwenda
kasi na ya umeme,” alisema King.
Katibu
mkuu wizara ya ujenzi, uchukuzi na mawasiliano (sekta ya uchukuzi) Dkt.
Leonard Chamuriho akizungumza katika hafla ya utiaji saini ujenzi wa
reli ya kiwango cha kimataifa (Standard gauge) kutoka Dar es salaam hadi
Morogoro unaotarajiwa kuanza hivi karibuni
Mwenyekiti
wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Miundombinu Mhe.Profesa
Richard Sigalla akizungumza katika hafla ya utiaji saini ujenzi wa reli
ya kiwango cha kimataifa (Standard gauge) kutoka Dar es salaam hadi
Morogoro unaotarajiwa kuanza hivi karibuni
Mkurugenzi
Mtendaji wa TRL,Masanja Kadogosa kwa kushirikina na Meneja wa Kanda ya
Africa Mashariki,Murat Hasim na Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya
Motaengil Africa,Manuel Antonio, wakisani mkataba wa ujenzi wa reli ya
kiwango cha kimataifa (Standard gauge) kutoka Dar es salaam hadi
Morogoro unaotarajiwa kuanza hivi karibuni.
0 comments :
Post a Comment