Pambano la fainali ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara, kati ya Mbao na wekundu wa Msimbazi, Simba lililopigwa Jumamosi katika uwanja wa Jamhuri, Dodoma limevunja rekodi ya mapato baada ya kuingiza shilingi milioni 117.
Kiasi hicho kimetokana na watazamaji takriban 15,000 waliokuwa na kiu ya pambano hilo la fainali lililomalizika kwa ushindi wa Simba wa mabao 2-1 uliopatikana kwenye muda wa ziada.
Rekodi ya mapato katika uwanja huo uluofanyiwa marekebisho katika dimba la kuchezea ilikuwa ni shilingi milioni 68.
Ukiondoa mechi za watani wa jadi, kiasi hicho ni kikubwa kuliko mapato ya mechi nyingine za Ligi na Kombe la Shirikisho zilizochezwa msimu huu.
Msimu huu mapato yameshuka kwa asilimia kubwa kiasi cha mechi kubwa kama Yanga na Mtibwa kushindwa kuingiza zaidi ya milioni 10 jijini Dar.
Baada ya mapato ya mechi za Dar kuporomoka sana , michezo ya mikoani inayohusisha Simba na Yanga ndio inaongoza kwa mapato makubwa huku rekodi ikishikiliwa na pambano baina ya Mbeya City na Simba lililoingiza kiasi cha shilingi milioni 60 Oktoba mwaka jana.Facebook