- Akizungumza na waandishi wa habari leo, Alhamis, Julai 20, mwanasheria wa chama hicho, Pamela Kihumo amesema mara nyingi wamekuwa wakipokea malalamiko kwa wapangaji ambayo yanatokana na baadhi ya madalali wasiotambulika kisheria.
- Dar es Salaam. Chama cha Wapangaji Tanzania (TTA) kimeiomba Serikali kuweka chombo maalumu kitakacho wadhibiti madalali wa nyumba ili kuondokana na migogoro inayotokea kati ya mpangaji na mpangishaji.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Alhamis, Julai 20, mwanasheria wa chama hicho, Pamela Kihumo amesema mara nyingi wamekuwa wakipokea malalamiko kwa wapangaji ambayo yanatokana na baadhi ya madalali wasiotambulika kisheria.
“Tunaiomba Serikali kuweka chombo kitakacho wadhibiti madalali ili kuweza kuwawezesha wapangaji kupata haki zao za kimsingi pindi wanapo kutana na chamgamoto na mwenye nyumba,” amesema Kihumu.
Amesema suala hilo linasababisha mpangaji kuvunjiwa mkataba kabla ya muda wake jambo ambalo linawatesa wapangaji ambapo wanaporudi kuwatafuta madalali hao wanakuwa wameshahama sehemu hiyo.
“Unakutana na dalali mitaani halafu wewe ni mgeni huwezi kujua kama nyumba hii ni nzuri lakini mwisho wa siku unaambiwa uondoke bila hata mkataba wako kwisha wakati hujajiandaa,” amesema Kihumu.
Pia, amesema endapo kutakuwepo na mamlaka ya kuwadhibiti madalali hao Serikali ingeweza hata kuwaandalia utaratibu na wa kulipa kodi kutokana na shughuli zao wanazozifanya.
Katibu Mkuu wa chama hicho, Ndumey Mukama anasema wakati mwingine wapangishaji wamekuwa na tabia ya kuwatoza kodi kubwa wapangaji ambapo ukiangalia nyumba yenyewe haina hata umeme wala sakafu.
“Unamkuta mpangishaji anakuambia lipia chumba kimoja Sh50,000 kwa mwezi wakati hakina hata maji ambapo hata kwenye mkataba wako unaona hivyo na ukigoma unalazimishwa uhame,”amesema Mukama.
Anasema kuwepo kwa chombo hicho kitasaidia kutoa mwongozo wa masuala ya upangaji kwa kuweka mikakati itakayosimamiwa na Serikali katika kuboresha hali ya upangishaji nchini.
Mukama anasema ili kuweza kuleta uwiano mzuri katika masuala ya ulipaji fidia kati ya mpangishaji lazima watu watakao fukuzwa kabla ya mkataba wao kumalizika wafanyiwe utaratibu wa kulipa fidia.
Pia, anasema viongozi wa Serikali za Mitaa na wadau mbalimbali wasaidie kumtetea mpangaji katika kusuluhisha migogoro inayotokea baina yao na wenye nyumba ili waweze kutambua haki zao
0 comments :
Post a Comment