Klabu ya Simba imesema kipa Aishi Manula hajakwenda nchini Afrika Kusini kuungana na kambi ya timu hiyo kwa sababu bado hajamaliza mkataba wake na Azam FC.
Mkuu wa idara ya habari na mawasiliano ya Simba SC, Haji Sunday Manara amesema kipa huyo atasajiliwa rasmi na kuungana na kikosi hicho muda wowote mkataba wake utakapomalizika mwishoni mwa mwezi huu.
Amewataja wachezaji wengine waliokwenda nchini humo jana wakitokea katika timu ya taifa, kuwa ni mabeki Erasto Nyoni, Shomari Kapombe waliosajiliwa kutoka Azam FC, Salim Mbonde na kipa Said Mohammed waliosajiliwa kutoka Mtibwa Sugar.
Wengine ni viungo, Muzamiru Yassin, Shiza Kichuya, Said Ndemla na mshambuliaji John Bocco ‘Adebayor’ aliyesajiliwa kutoka Azam FC.
Simba itarejea Dar es Salaam siku chache kabla ya tamasha lao la kila mwaka la ‘Simba Day’, lililopangwa kufanyika kama kawaida Agosti 8 mwaka huu katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika tamasha hilo, Simba itatambulisha kikosi chake kamili cha msimu kabla ya kucheza mechi ya kirafiki na timu moja kutoka nje ya Tanzania baada ya burudani mbalimbali ikiwemo zoezi la kuwauzia jezi mpya wapenzi na wanachama wa timu hiyo.


0 comments :
Post a Comment