Mbowe akosoa wawekezaji kupokwa viwanda

Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe amekosoa hatua ya serikali ya Tanzania kuwapokonya viwanda wawekezaji walioshindwa kuviendeleza na badala yake ameitaka kuweka mazingira rafiki kwa ajili ya watu binafsi kuendesha viwanda hivyo.
Akizungumza na wanahabari leo wakati akitoa maazimio ya kikao cha kamati kuu ya chama hicho, Mbowe amesema serikali haina uwezo wa kuviendesha viwanda hivyo kwa kuwa haina fedha na haifanyi biashara, hivyo inapaswa kuwaachia watu binafsi wenye uwezo wa kuviendesha ili kuimarisha uchumi wa nchi.
Amesema serikali inapaswa kwanza kufanya uchambuzi ili kubaini sababu za watu waliobinafsishiwa viwanda kushindwa kuviendeleza kabla ya kuwapokonya kwa kuwa uamuzi wa kuwapokonya bila kuwatengenezea mazingira ya wao kutengeza faida ni sawa na kuua sekta binafsi nchini.
Akizungumzia sababu za viwanda vingi kufa, Mbowe amesema wafanyabiashara hao wameshindwa kuviendesha kwa kuwa walikuwa hawapati faida kutokana na vikwazo vya kibishara kutoka serikalini pamoja na mlolongo mrefu wa urasimu katika mchakato wa uwekezaji kwenye sekta hiyo ya viwanda.
“Hakuna mfanyabiashara duniani ambaye atapewa kitega uchumi au kiwanda ambacho kitampa faida halafu akakifunga eti kwa sababu tu anaichukia Tanzania…. Ukinipa kiwanda ambacho kinanipa faida siwezi nikakifunga…… Lakini pia rais anapaswa kutambua kuwa hata kubadilisha biashara ni sehemu ya biashara, kiwanda cha kandambili miaka iliyopita siyo lazima kizalishe kandambili hadi leo…. Sijalaani rais kurejesha viwanda, nimezungumza economic facts,”amesema Mbowe.
Pia Mbowe amesema tangu serikali ya awamu ya tano iingie madarakani, sekta ya viwanda imeporomoka na kwamba viwanda vinavyozinduliwa hivi sasa uwekezaji wake wa mitaji ulifanyika wakati wa serikali ya awamu ya nne.
“Kwa mujibu wa takwimu za Benki Kuu, mwaka huu mikopo ya kibenki katika sekta ya viwanda ni 0%, ikimaanisha kuwa hakuna uwekezaji kwenye sekta ya hiyo,” amebainisha Mbowe.
Katika hatua nyingine Mwenyekiti huyo wa CHADEMA ambaye pia ni mbunge wa Hai mkoani Kilimanjaro, amesema chama hicho kinapinga kile alichodai kuwa ni sera za serikali kutaka kuirudisha Tanzania katika ujamaa kwa kudhoofisha sekta binafsi na kuamini kuwa kila mtu anayepata pesa kupitia sekta binafsi ni ‘mpiga dili.’
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment