Serikali ya Tanzania imepata sifa kubwa katika mkutano wa 72 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaoendelea New York, Marekani kutokana na utendaji mzuri wa serikali ya Rais John Magufuli kushughulikia masuala mbalimbali yenye tija kwa wananchi pamoja na matumizi mazuri ya fedha ya walipa kodi.
Akizungumza kutoka New York anakomwakilisha Rais, Waziri wa Mambo ya Nje, Dkt. Augustine Mahiga amesema Tanzania imekuwa kivutio katika viunga vya Umoja wa Mataifa kutokana na mtindo wa utendaji unaolenga kuwakomboa na kuwaletea huduma bora wananchi.
Dkt. Mahiga amesema viongozi mbalimbali aliokutana nao katika mkutano huo kutoka nchi za Afrika, Asia, Ulaya na Marekani wameonyesha kuvutiwa na utendaji wa rais Magufuli na kusema nchi zao ziko tayari kumualika au viongozi wao wako tayari kuja Tanzania ili kupata uzoefu wa namna rais Magufuli anavyofanya mageuzi katika kipindi kifupi huku wakimwona kuwa mtu jasiri na mwenye upeo katika kuwatumikia watu wake.
Kudhihirisha hilo, Balozi Dkt. Mahiga amesema mpaka sasa ameshafanya mikutano ya nchi na nchi au taasisi mbalimbali ipatayo 25 mbali na kuhutubia kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Aidha kivutio kingine katika mkutano huo ni udogo wa ujumbe wa Tanzania. Mbali na Dkt. Mahiga ujumbe wake una maafisa wengine watatu kutoka wizarani kwake wakiungana na Balozi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Modest Mero.
Akizungumzia ukubwa wa ujumbe aliouongoza, Waziri Mahiga anasema hii ni historia nyingine kwani katika mikutano ya Umoja wa Mataifa, Tanzania imekuwa na ujumbe usiopungua watu 40 na wakati fulani walipata kufikia wajumbe 100; lakini sasa maafisa wachache wametekeleza kazi kwa ufanisi.
Akihutubia Baraza Kuu, pamoja na kutoa salama maalum za rais Magufuli, Waziri Mahiga amefafanua mageuzi mbalimbali yanayoendelea nchini hasa mapambano dhidi ya rushwa na kuimarisha uwajibikaji na akasisitiza utayari wa Tanzania kuendelea kushirikiana na Umoja wa Mataifa.Facebook