Klabu ya Simba imelalamikia idadi ndogo ya mipira inayokuwepo uwanjani wakati wa michezo inayocheza katika viwanja vya ugenini.
Mkuu wa habari na mawasiliano wa klabu hiyo, Haji Manara ametolea mfano mchezo kati ya Mbao na Simba uliopigwa Alhamisi iliyopita katika dimba la CCM Kirumba jijini Mwanza, akidai kuwa huo ulikuwa ni moja ya mkakati wa kuchelewesha muda.
Manara amesema katika mchezo ule palikuwa na mipira isiyozidi minne, jambo ambalo lilikuwa likilazimu wachezaji kusubiri kwa muda mrefu pindi mpira unapotoka nje, jambo ambalo linaweza kuwa limechangia kuwanyima ushindi.
“Siyo kwamba tunalalamika, bali tunatoa tahadhari katika michezo ijayo, uwanjani kuwe na mipira ya kutosha, haiwezekani mchezo wa ligi kuu kuwe na mipira minne uwanjani…. Na katika mchezo ujao na Stand hili suala tutalizungumza mapema wakati wa pre-match meeting,” amesema Manara.
Mbali na suala la idadi ya mipira, Manara pia amelalamikia uamuzi katika mchezo huo dhidi ya Mbao FC akidai Simba kunyimwa penati baada ya John Bocco kufanyiwa madhambi ndani ya eneo la hatari.
Katika hatua nyingine msemaji huyo machachari wa Simba ameziasa timu mbalimbali za mikoani kutokamia vilabu vikubwa pekee kwa kufanya “mchezo michafu”, bali wadau wa soka katika mkoa husika wanapaswa kuwa na mikakati ya muda mrefu katika mechi zote za ligi.
Kuelekea katika mchezo wao unaofuata na Stand United utakaopigwa Jumapili ijayo mkoani Shinyanga, Simba imepiga kambi jijini Mwanza ambapo kwa mujibu wa Manara, kikosi kiko katika hali nzuri.



0 comments :
Post a Comment