Ugumu kuhusiana na urejeshwaji huo unaelezwa kutokea baada ya mamlaka mbalimbali kujiweka mbali na fedha hizo, zikiwamo Wizara ya Fedha na Mipango na pia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Julai 10, mwaka huu, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini katika serikali ya awamu ya nne, William Ngeleja, alitangaza kurejesha Sh. milioni 40.4 zilizohusishwa na sakata hilo, ambazo alikiri kupewa na mmoja wa watuhumiwa Februari 12, 2014 kwa nia njema ya kusaidia shughuli za maendeleo katika jimbo la Sengerema ambalo yeye ni Mbunge.
“Nimeamua kurejesha fedha hizi hata kama aliyenipa msaada bado ni mtuhumiwa, kwa vile hajathibitika kupatikana na hatia, kwa sababu sitaki kuwa sehemu ya kashfa au tuhuma hizo.
“Nimesononeshwa na kufadhaika sana kuona kuwa msaada niliopewa sasa unahusishwa na tuhuma,” alisema Ngeleja alipozungumza na waandishi wa habari wakati akitangaza kurejesha fedha hizo serikalini kupitia malipo aliyodai kuyafanya katika Benki ya CRDB, Tawi la PPF Tower.
“Fedha hizo nilizipokea kwa nia njema kama msaada au mchango, ili zinisaidie kutimiza majukumu yangu ya kibunge, hususan kusaidia wananchi wa jimbo langu na taifa kwa ujumla. Nilizipokea bila kujua kwamba zinahusishwa na kashfa ya akaunti ya fedha za Escrow kama ilivyo sasa,” aliongeza Ngeleja katika taarifa yake hiyo aliyoitoa Julai 10, 2017.
Aidha, Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Bukoba, Dk. Methodius Kilaini, pamoja
na Eusebius Nzigilwa, Askofu msaidizi wa kanisa hilo Jimbo Kuu la Dar es Salaam, walikaririwa kutoa taarifa Septemba 7, mwaka huu, wakielezea dhamira yao ya kurudisha fedha walizoingiziwa kwenye akaunti zao mwaka 2014 kwa ajili ya shughuli za kiroho na mmoja wa watuhumiwa wa sakata la Escrow.
Ilielezwa kuwa viongozi hao wa dini waliamua kurudisha fedha hizo kutokana na kuwapo kwa kesi mahakamani ya tuhuma ya uhujumu uchumi inayomkabili mtu aliyewapa fedha hizo.
Kwa mujibu wa mijadala ya Bunge, Kilaini aliingiziwa Sh. milioni 80.5 huku Askofu Nzigilwa akidaiwa kupata Sh. milioni 40.4