Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imewafikisha Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani Mwanza washtakiwa watatu kwa tuhuma za kughushi namba tambulishi za simu (IMEI) kwa lengo la kuzipatia namba hizo utambulisho mpya jambo ambalo ni kosa kisheria. Wakisomewa mashtaka hayo juzi na mawakili wa Serikali Jackline Nyantori na Jehovaness Zacharia mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi Mkoa wa Mwanza Wilbert Chuma, washitakiwa hao Isaya Lucas na Daudi Masesa walidaiwa kutenda kosa hilo Agosti 17 mwaka huu jijini Mwanza.
Mshtakiwa mwingine aliyesomewa mashtaka hayo na wakili wa Serikali Emma Gelano ni Faraji Said mbele ya hakimu mkazi Gwayi Sumaye.
Ilidaiwa kuwa washtakiwa hao walitenda kosa hilo kinyume na sheria namba tatu ya mawasiliano ya kielektroniki na posta ya mwaka 2010 kifungu cha 154 na 135.
Alidai washtakiwa walitenda kosa hilo kwa nyakati tofauti wakibadilisha IMEI za namba za siri za simu mbalimbali ili kuzitengeneza namba tambulishi mpya huku akidai upelelzi wa shauri hilo umekamilika.
Washtakiwa waliachiwa huru baada ya kukidhi masharti ya dhamana ambayo ilikuwa ni kila mtuhumiwa kuwa na mdhamini mmoja atakayesaini mali kauli ya Sh10 milioni, akiwa na barua ya utambulisho kutoka kwenye uongozi wa mtaa au kata na kitambulisho binafsi cha mpiga kura au leseni ya udereva.
Shauri hilo liliahirishwa hadi Desemba 18 watuhumiwa watakapoanza kusomewa hoja za awali.
0 comments :
Post a Comment