Kiongozi wa kitaifa wa mradi wa CFIT, Prof. Ralph Masenge
akimkaribisha mgeni rasmi Kaimu Kamishina wa Elimu, Benjamin Kulwa
(hayupo pichani) kufungua kongamano linalohusu upitiaji wa waraka wa
mafunzo ya Tehama kwa wakufunzi wa vyuo vya ualimu linalofanyika mjini
Bagamoyo.
Kaimu Kamishina wa Elimu, Benjamin Kulwa akisoma hotuba kwa
niaba ya Kamishina wa Elimu, Profesa Eustella Bhalusesa wakati akifungua
rasmi kongamano linalohusu upitiaji wa waraka wa mafunzo ya Tehama kwa
wakufunzi wa vyuo vya ualimu linalofanyika mjini Bagamoyo. Kulia ni
Ofisa Miradi ya Mawasiliano, Habari na Tehama wa Shirika la Kimataifa la
Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO) nchini, Al Amin Yusuph.
Pichani juu na chini ni washiriki wa kongamano linalohusu
upitiaji wa waraka wa mafunzo ya Tehama kwa wakufunzi wa vyuo vya ualimu
wakati kongamano hilo likiendelea mjini Bagamoyo.
Kiongozi wa kitaifa wa mradi wa CFIT, Prof. Ralph Masenge
(kushoto) akijadili jambo na mgeni rasmi Kaimu Kamishina wa Elimu,
Benjamin Kulwa (katikati). Kulia ni Ofisa Miradi ya Mawasiliano, Habari
na Tehama wa Shirika la Kimataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni
(UNESCO) nchini, Al Amin Yusuph.
Kiongozi wa kitaifa wa mradi wa CFIT, Prof. Ralph Masenge
(kulia), akifurahi jambo na Ofisa Miradi ya Mawasiliano, Habari na
Tehama wa Shirika la Kimataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO)
nchini, Al Amin Yusuph (katikati) pamoja na Mratibu wa kitaifa wa mradi
wa CFIT kutoka UNESCO, Faith Shayo (kushoto) mara baada ya kufunguliwa
rasmi kwa kongamano linalohusu upitiaji wa waraka wa mafunzo ya Tehama
kwa wakufunzi wa vyuo vya ualimu.
Mgeni rasmi Kaimu Kamishina wa Elimu, Benjamin Kulwa (walioketi
wa pili kushoto) katika picha ya pamoja na washiriki wa warsha hiyo
inayomalizika leo mjini Bagamoyo.
Na Mwandishi wetu, Bagamoyo
KAMISHINA wa Elimu, Profesa Eustella Bhalalusesa amesisitiza
haja ya kuhakikisha kwamba viwango vya umahiri vya Tehama kwa wakufunzi
wa vyuo vya ualimu nchini vinakua vya juu kukidhi haja ya matumizi ya
kufundishia na kujifunza nchini.
Alitoa kauli hiyo mjini hapa wakati
akifungua kongamano linalohusu upitiaji wa waraka wa mafunzo ya Tehama
kwa wakufunzi wa vyuo vya ualimu.
Katika hotuba yake iliyosomwa na Kaimu
Kamishina wa Elimu, Benjamin Kulwa alisema kwamba changamoto ya Tehama
inaonekana wazi katika matumizi yake na hivyo wakufunzi lazima wawe
mahiri.
"Duniani kote, sekta ya uchumi, fani
mbalimbali, taasisi na hata mifumo ya maisha yanategemea sana matumizi
ya Tehama kwa sasa. Kadhalika, maendeleo makubwa katika Tehama
yamebadili namna mambo yanavyofanyika,” alisema.
Alisema kwa kuhakikisha kwamba kuna
maendeleo ya kutosha ni vyema walimu kuwa na umahiri unaotakiwa kwani
Tehama inachangamoto nyingi zinazotakiwa kuangaliwa ili kuweza kuitumia
ipasavyo kuleta mabadiliko katika jamiii.
Aliwataka washiriki kuhakikisha kwamba
wanapitia muswada huo kwa makini na kujazia maeneo yote ambayo wataalamu
wameshindwa kumaliza na kusaidia kuweka mtaala huo vyema kwa mafunzo.
Kongamano hilo ambalo ni sehemu ya mradi wa
kuimarisha uelewa kwa wanafunzi na wakufunzi vyuo vya walimu ili
kuboresha matumizi ya Tehama katika mafunzo hasa masomo ya sayansi
limeshirikisha wataalamu mbalimbali na kuendeshwa na Shirika la Umoja wa
Mataifa la Elimu Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwa kushirikiana na watu
wa China.
Alisema kwamba serikali inatambua kuwa Tehama inaweza kutumika vyema katika kubadili na kuboresha mfumo wa elimu Tanzania.
Aidha alisema Sera mpya ya elimu na mafunzo
ya mwaka 2014 inatambua umuhimu wa Tehama katika kuboresha viwango vya
elimu nchini Tanzania.
Alisema moja ya malengo ya sera ni kuonesha
mahitaji halisi ya Tehama nchini katika upande wa wataalamu na vifaa ili
kufanikisha utoaji wa elimu hata ya masafa katika ngazi zote.
Kongamano hilo ni moja ya mradi wa China
Funds in Trust Project (CFIT) wa UNESCO na serikali ya China wenye lengo
la kusaidia serikali ya Tanzania kuimarisha umahiri wa wakufunzi na
walimu kwa kuwawezesha kujua tehama na kuitumia.
Mradi huo umelenga kuongeza uwezo wa vyuo
vya walimu na teknolojia ya kisasa ya Tehama na vifaa vyake ili kusaidia
kujifunza na kufunza.
Ingawa kwa sasa vyuo vinavyofanyiwa kazi na
mradi huo vipo viwili vipo vingine vinane vinavyofunza walimu wa sayansi
na hesabu vitaingizwa.


0 comments :
Post a Comment