Na Mwashungi Tahir -Maelezo Zanzibar
………………………………
Katibu Mtendaji Baraza la
Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) Mwanahija Haji Juma amesema kwamba jamii
inahitaji kuhamasishwa kuthamini na kuenzi Utamaduni wa Zanzibar ili
uweze kuimarika na kukua zaidi .
Hayo ameyasema leo huko katika
Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) Kampasi ya Vuga
alipokuwa akifungua Kongamano la Tamasha la 20 la Utamaduni la
Mzanzibari lililohudhuriwa na wanafunzi wa Vyuo Vikuu mbali mbali
nchini.
Amesema Kongamano hilo ambalo ni
mfululizo wa Tamasha la Zanzibar lililozinduliwa rasmi na Makamu wa
Pili wa Rais tarehe 21 katika Ukumbi wa Salama Bwawani linasisitiza
kuendelezwa, kuenziwa na kuthaminiwa na watu wote.
“Tamasha hili lilianzishwa
nakuszinduliwa rasmi na Rais wa awamu ya tano Mh. Salmin Amour Juma
mwaka 1994 katika Uwanja wa Amani,”alisema Katibu Mtendaji.
Aidha alisema lengo kuu la Tamasha
hilo linalofanyika kila mwaka ni kulinda, kuenzi na kuwahamasisha
wananchi kuelewa Utamaduni wao kwa undani zaidi kwani ni kioo cha
wananchi.
Amesema Utamaduni ni mfumo wa
maisha wa jamii husika na sio ngoma pekee kwani yapo mambo mengi
katika utamaduni yakiwemo mavazi, vyakula , malezi , kusoma vitabu vya
historia, kutunga mashairi na mengineo.
Nae Mkuu wa Idara ya Kiswahili wa
SUZA Dkt. Maulid Omar amesema iko haja ya wananchi kufahamu changamoto
zinazokabili Utamaduni wa Zanzibar kwani baadhi ya mambo yanaingizwa
kuharibu utamaduni huo.
Mada mbili ziliwasilishwa na
kujadiliwa katika Kongamano hilo ambazo ni athari za Utalii katika
kuendeleza Utamaduni iliyotolewa na Bi. Mwanahamisi Hassan wa Idara ya
sayansi jamii SUZA na mada ya pili iliyotolewa na Mhadhiri Msaidizi
Omar Salum Mohd ilizungumzia mshikamano wa Utamaduni na Uisilamu.
Kongamano hilo lilifungwa na
Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili Bi. Mwanahija Haji Juma na
kauli mbiu ya Tamasha la mwaka huu ni Utamaduni kwa Furaha, Amani na
Utulivu.


0 comments :
Post a Comment