Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania
(PTA), Awadh Massawe akizungumza na wanahabari wakati akikabidhi hundi
ya sh.milioni mbili kwa Taasisi ya Habari Development Association Dar es
Salaam jana asubuhi.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Usimamizi wa Bandari Tanzania (PTA), Awadh Massawe (kushoto),
akikabidhi mfano wa hundi ya sh.milioni mbili kwa Mkurugenzi wa Taasisi
ya Habari Development Association (HDA), Kunze Mswanyama (kulia), Dar es
Salaam jana asubuhi kwa ajili ya kuandaa mafunzo ya kuwawezesha
waandishi wa habari kujenga weledi wa kufanya tafiti na kuandika habari
za kupambana na ujangili. Wa pili kushoto ni Ofisa Mwandamizi wa
Mawasiliano wa TPA, Focus Mauki na Katibu Mkuu wa Taasisi hiyo, Benard
James.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Habari Development Association (HDA), Kunze
Mswanyama (kulia), akizungumzia kuhusu mafunzo na umuhimu wa wanahabari
katika kupambana na ujangili wa rasilimali za taifa kabla ya kukabidhiwa
msaada wa sh.milioni 2 kutoka PTA. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa PTA,
Awadh Massawe.
Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), imetoa sh. milioni 2 kwa
Taasisi ya Habari Development Association kwa ajili kuandaa mafunzo ya
kuwawezesha waandishi wa habari kujenga weledi wa kufanya tafiti na
kuandika habari za kupambana na ujangili.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Awadh Massawe alikabidhi hundi ya thamani
ya fedha hizo kwa Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Kunze Mswanyama jijini Dar
es Salaam jana.“Tunaunga mkono juhudi hizi za kupambana na ujangili,”
alisema Massawe.
Alisema TPA imefanya hivyo kwa kuwa nchi ina tatizo la uwindaji haramu
hasa wa ndovu na usafirishaji wa pembe za ndovu na kulisababishia hasara
taifa kupitia mipaka yake.
Alifafanua kuwa bandari ya Dar es Salaam ni sehemu ya mpaka wa taifa,
hivyo lazima TPA iunge mkono juhudi za kuelimisha jamii na kuzuia
uhalifu huo.
Massawe alisema kwa sasa wanatarajia kufunga kamera 400 za CCTV ili
kuimarisha ulinzi na kuwa skana tatu zimeletwa bandarini kwa ajili
yakuziongezea nguvu skana mbili zilizopo.
Pia, alisema wanatarajia kupata msaada wa mbwa maalumu wa ulinzi
watakaotolewa na Serikali ya Marekani. Alisema TPA inaendelea kuwajengea
uwezo wafanyakazi kimaadili ili kuendelea kufanya kazi kwa weledi na
uaminifu kwa faida ya taifa.
Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Mswanyama alisema fedha walizopewa
watazitumia kwa kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari 54 kwa masuala ya
ujangili kupata weledi na kutafiti na kufichua ujangili. “Tunahitaji
kujenga uwezo wa kupambana na ujangili ili taifa liweze kunufaika
nazo,” alisema. (Imeandaliwa na mtandao wa www. habari za jamii.com-simu namba 0712-727062)


0 comments :
Post a Comment