Meneja wa NHIF mkoa wa Singida, Agnes Chaki (kushoto) akimkabidhi
Mkuu wa wilaya ya Singida, Alli Amanzi msaada wa mashuka 200 kwa ajili
ya hospital ya mkoa mjini hapa.(Picha na Nathaniel Limu).
Mkuu wa wilaya ya Singida,Alli Amanzi (kulia) akibadilishana mawazo
na Meneja Mfuko wa taifa wa bima ya afya (NHIF) mkoa wa Singida, Agnes
Chaki (katikati) muda mfupi kabla Meneja NHIF hajakabidhi mashuka 200
kwa hospitali ya mkoa mjini hapa.Kushoto ni Afisa uthibiti ubora wa
huduma NHIF mkoani hapa, Dk.Edwin Mwangajilo.
Na Nathaniel Limu, Singida
HOSPTALI ya mkoa wa Singida iliyopo mjini
hapa,inakabiliwa na uhaba mkubwa wa mashuka kitendo kinachochangia
wagonjwa kutumia mashuka yao binafsi wakati wote wanapokuwa wamelazwa
hospitalini hapo.
Hayo yamesemwa na Kaimu mganga mkuu wa mkoa
wa Singida,Dk.Henry Mgetta, wakati akizungumza kwenye hafla ya
makabidhiano ya msaada wa mashuka 200 yaliyotolewa msaada kwa hospitali
ya mkoa na mfuko wa taifa wa bima ya afya (NHIF) mkoani Singida.
Alisema hospitali hiyo yenye vitanda 300 vya kulaza wagonjwa,inakabiliwa na uhaba wa mashuka 2,400 na magodoro 230.
“Hali ni mbaya mno,shuka 100 tulizonazo,ni
chakavu na kwa ujumla nazo hazifai kwa matumizi ya binadamu.Wagonjwa
wanaolazwa inawalazimu kutumia shuka zao binafsi jambo ambalo
halikubaliki”,alisema Dk.Mgetta.
Alisema mbali na uhaba wa shuka na
magodoro,hosptali hiyopia ina uhaba wa vitanda na hasa kwenye wodi ya
wazazi, kitendo kinachochangia wajawazito wanne watumie kitanda kimoja.
“Natoa wito kwa wadau mbalimbali,waangalie
uwezekano wa kuisaidia kwa hali na mali hospitali yetu hii na vituo
mbalimbali,ili viweze kutoa huduma bora inayokidhi mahitaji ya
wananchi”’alisema Dk.Mgetta.
Kwa upande wake Meneja wa NHIF mkoa wa
Singida, Agnes Chaki,alisema kuwa wametoa msaada huo wa mashuka hayo
baada ya kuombwa na serikali ya wilaya ya Singida.
Alisema majukumu ya NHIF,ni pamoja na
kuhakikisha vituo vya kutolea huduma za afya zinajitosheleza kwa kuwa na
mahitaji yote muhimu kwa kutoa misaada na vile vile mikopo ya kununulia
dawa,vifaa tiba na uboreshaji wa majengo.
“Nina imani kituo cho chote cha
afya,zahanati na hospitali,kinapokuwa na vitanda,mashuka na mambo
mengine muhimu kwa wagonjwa wanaolazwa,kitendo hicho kitakuwa
kinawajengea mazingira mazuri ya kuendelea na matibabu bila usumbufu wo
wote”,alifafanua meneja huyo.
Chaki alisema NHIF itaendelea kutoa misaada
mbalimbali kadri uwezo utakavyoruhusu kwa lengo la kusaidiana na
serikali katika kuboresha utoaji wa huduma za afya.
0 comments :
Post a Comment