![]() |
| Meneja Uhusiano wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Nicodemus Mushi akizungumza na vyombo vya habari Makao Makuu ya TTCL jijini Dar es Salaam kujibu madai ya TEWUTA. |
KAMPUNI ya Simu Tanzania (TTCL)
imepinga madai yaliyotolewa na Chama cha Wafanyakazi wa Sekta ya Huduma
za Mtandao wa Mawasiliano Tanzania (TEWUTA) jana dhidi ya Menejimenti na
Bodi ya Wakurugenzi ya TTCL na kufafanua kuwa madai hayo si ya kweli
zaidi ya upotoshaji wenye nia ovu ya kufanikisha malengo binafsi na
kutaka kuikwamisha jitihada za TTCL katika maendeleo.
Meneja Uhusiano wa TTCL,
Nicodemus Mushi akizungumza na vyombo vya habari leo Makao Makuu ya
kampuni hiyo jijini Dar es Salaam alisema madai yaliyotolewa na Chama
cha TEWUTA dhidi ya Menejimenti na Bodi ya Wakurugenzi ya TTCL hayana
ukweli wowote bali wahusika walilenga kuupotosha umma.
“Menejimenti ya Kampuni ya Simu
Tanzania (TTCL), inapenda kuujulisha Umma kuwa, madai yaliyotolewa na
Chama cha TEWUTA dhidi ya Menejimenti na Bodi ya Wakurugenzi ya TTCL si
sahihi. Hoja hizo zimejikita katika upotoshaji wenye nia ovu ya
kufanikisha malengo binafsi ya wahusika na kukwamisha jitihada kubwa
zinazofanywa na Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Bodi ya
Wakurugenzi, Menejimenti na Wafanyakazi wa TTCL wenye nia na malengo ya
kutekeleza mpango mkakakti wa kuiboresha na kuiimarisha Kampuni ya Simu
Tanzania.
Akifafanua zaidi Meneja Uhusiano
huyo wa TTCL alisema mwaka 2007 Kampuni ya Simu Tanzania ilifanya
mabadiliko ya Muundo wa Kampuni ili kuendana na hali ya soko la
Ushindani katika sekta ya mawasiliano na Muundo uliopo sasa ni ule
uliopitishwa na kuanza Kutumika mwaka 2007 baada ya kuidhinishwa na
kupitishwa na Bodi ya Wakurugenzi.
Alisema menejimenti mpya ya TTCL
iliyoanza kazi Februari 2013 iliainisha changamoto mbalimbali za
kibiashara na kutengeneza Mpango Mkakati utakaoletab mabadiliko ya
kibiashara na kuongeza tija, huku ikizingatia mabadiliko ya Kibiashara
na ushindani wa soko katika sekta ya mawasiliano, Menejimenti iliomba
na kupata kibali cha Bodi ya Wakurugenzi wa TTCL kumtafuta Mshauri
mwelekezi kwa njia ya Zabuni ili kupitia na Kushauri juu ya Muundo Mpya
wa Kampuni utakaoendana na Mahitaji ya Kibiashara na kuleta ufanisi.
Aliongeza kuwa matokeo ya Kazi ya
Mshauri mwelekezi yamelenga kubadilisha muundo wa Kampuni, Muundo wa
Mishahara na Muundo wa utumishi. Mpango huu wa Mabadiliko ya Kibiashara
unategemewa kukamilika katika kipindi cha mwaka 2016. Aidha alifafanua
kuwa muundo wa mishahara unaotumika hivi sasa ni ule uliopitishwa Mwaka
2007 baada ya Kubadilika kwa Muundo wa Kampuni kama ulivyoidhinishwa na
Bodi ya Wakurugenzi wa TTCL.
“…Mfumo huu uliiweka TTCL katika
nafasi ya kukabiliana na soko la ajira kimaslahi. Mfumo huu wa Mishahara
ulizingatia pia matakwa ya kisheria ambapo kwa mujibu wa Sheria ya
Ajira na Mahusiano Kazini Namba 6/2004 zimeainishwa aina tatu za
Mikataba ya Ajira. Yaani: Mkataba wa Ajira usiokuwa na Muda Maalumu
(Unspecified period of time), Mkataba wa Ajira wa Muda Maalum (Fixed
Employment contracts) na pia Mkataba wa Ajira wa kazi Maalum (Special
Task)…”
“…Hivyo Muundo wa Mishahara
uliopitishwa mwaka 2007 uliainisha madaraja ya malipo na viwango husika
ikiainisha aina ya mkabata, Mkataba wa Ajira usiokuwa na Muda Maalum na
Mkataba wa Ajira wa Muda Maalum. Katika muundo huu madaraja na ngazi za
Mishahara zimegawanyika katika ngazi Kumi (10) kuanzia TTCL 1 (Ikiwa
ndio Kiwango cha Juu) hadi TTCL 10 (Ikiwa ndio kiwango kidogo) Muundo
huu uko wazi na ndio unaotumika kulipa mshahara ya wafanyakazi wote wa
Kampuni ya Simu Tanzania. Hakuna ulipaji wa mishahara (Payroll) yoyote
ya Siri inayotumika tofauti na hiyo iliyoainishwa,” alifafanua Meneja
Uhusiano huyo katika taarifa yake.
![]() |
| Meneja Uhusiano wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Bwana Mushi akifafanua masuala mbalimbali katika mkutano huo na vyombo vya habari. |
Akizungumzia kuhusu Bodi ya
Wakurugenzi ya TTCL alisema imekuwa na mchango mkubwa katika kusukuma
maendeleo ya TTCL chini ya uenyekiti wa Dk. Enos Bukuku na baadae chini
ya Mwenyekiti wa muda Jaji Joseph Sinde Warioba.
Aliyataja baadhi ya mambo mengi
yaliofanywa na Bodi hiyo kuwa ni pamoja na kuondoka kwa Mbia Mwenza
Bharti Airtel na pia kuishauri Serikali juu ya umuhimu wa kuondoka kwa
Bharti Airtel ndani ya TTCL ili kuwezesha juhudi za dhati za kuifufua
TTCL.
“..Bodi imetoa ushauri, miongozo
na maelekezo kwa menejimenti, imeshiriki vikao vya majadiliano ya
kuondoka kwa Bharti Airtel na kipekee, imefanya mawasiliano na ofisi za
Serikali zikiwepo Ofisi ya Rais na Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia kusisitiza umuhimu wa Kuondoka kwa Bharti Airtel. Juhudi hizi
zimechangia sana kusukuma swala hili ambalo kwa sasa liko katika hatua
za mwisho…,” alisema Bwana Mushi.
Bodi ya wakurugenzi ilipitisha
uamuzi wa TTCL kuingia katika mradi ya mabadiliko wa mfumo wa kibiashara
ili TTCL iweze kupanua mtandao wake na kuwa wa kisasa zaidi kuweza
kutoa huduma mbalimbali kwa teknolojia ya kisasa (GSM, UMTS & LTE)
zikiwemo huduma za simu za mkononi na mawasiliano ya data kwa ufanisi
zaidi ili Kampuni iweze kukabiliana na ushindani ulioko sokoni na
kuongeza pato lake. Tayari sehemu ya mradi huo imekamilika (4G LTE) ya
kutoa huduma ya data kwa kiwango cha juu katika sehemu ya maeneo kadhaa
ya Dar es Salaam. Utekelezaji wa mradi utaendelea kwa sehemu zingine.
Kwa kushirikiana na Serikali Bodi
inaendelea kutoa ushirikiano stahiki katika hatua za kuiboresha TTCL
zikiwemo kuhakikisha TTCL inapata mtaji wa kutosha kuendesha shughuli za
mawasiliano ndani na nje ya nchi kuweza kuendana na Sera za Taifa na
kuboresha pato la Kampuni. Bodi imekua ikitoa mchango mkubwa
kuhakikiksha Mkongo wa Taifa unaendeshwa vizuri kwa kuwa na mawasiliano
wakati wote. Aidha, sambamba na maamuzi ya Baraza la Mawaziri juu ya
TTCL kumilikishwa Mkongo wa Taifa, Bodi ya Wakurugezi imetoa mchango
mkubwa juu ya ufuatiliaji wa swala hili kwenye Wizara husika. Serikali
kupitia wizara hya Mawasiliano iko katika hatua nzuri katika kukamilisha
swala hili.” Alieleza katika taarifa yake.
![]() |
| Baadhi ya wanahabari wakifuatilia mazungumzo hayo. |
Akizungumzia Kampuni ya Rubiem
ambaye ni Mshauri mwelekezi aliyepatikana kwa kufuata taratibu sahihi za
manunuzi ya Umma, alisema mchango wa kampuni hiyo katika mpango wa
mageuzi kibiashara ni mkubwa na unaonekana dhahiri tofauti na madai
yaliyotolewa.
“…Matokeo ya kazi yake yataanza
kuonekana mwishoni mwa mwaka huu ambapo huduma na bidhaa mpya zitaingia
sokoni. Mshauri huyu anatarajia kukamilisha kazi yake katika robo ya
kwanza ya mwaka 2016. Ieleweke pia kwamba, hatua ya Menejimenti
kumuongezea muda mshauri huyu hazihusishi gharama zozote za nyongeza nje
ya mkataba wake wa kazi na TTCL.
Menejimenti ya Kampuniya Simu Tanzania TTCL inaomba kutumia
fursa hii kuwajulisha Umma kwamba, hali ya Kampuni yao ni thabiti,
utendaji wa kazi unaendelea vizuri na jitihada mbali mbali za kuboresha
huduma zinaendelea kwa ufanisi mkubwa,” alifafanua Bwana Mushi kwa
wanahabari.
“…Menejimenti ya Kampuniya Simu
Tanzania TTCL inapenda kuujulisha Umma kuwa, oja zote zilizotolewa na
TEWUTA si za kweli, ni taarifa zilizopotoshwa kwa makusudi, zikilenga
kufanikisha malengo binafsi na kukwamisha jitihada kubwa zinazofanywa na
Wizara ya Sayansi na Mawasiliano, Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni,
Menejimenti na Wafanyakazi wa TTCL wenye lengo la kuifanya Kampuni
kutimiza kikamilifu Wajibu wake kwa Umma. Ieleweke pia kwamba, Muundo wa
mishahara ya Watumishi wa Kampuni ya simuTanzania TTCL uko wazi na ndio
unaotumika kulipa mshahara ya wafanyakazi wote wa Kampuni ya Simu
Tanzania. Ofisi inayolipa mishahara ya wafanyakazi wote wa TTCL iko
idara ya Fedha na kusimamiwa na wafanyakazi wa Kampuni ya Simu. Hakuna
Payroll yoyote ya Siri inayotumika tofauti na hiyo iliyoainishwa, hakuna
posho zozote zinalipwa kinyume na utaratibu.” alieleza Meneja huyo wa
TTCL.






0 comments :
Post a Comment