Awataka waliohamia kambi ya pili warudi kundini
Asema anataka kuleta maendeleo kwa wana-Ruangwa
WAZIRI MKUU Kassim
Majaliwa amesema hana kinyongo na mtu yeyote kwa sababu alitangaza
msamaha siku aliyokabidhiwa cheti kuwa mbunge wa jimbo la Ruangwa na
kusisitiza kuwa siasa ziliisha tangu Oktoba 25, mwaka huu.
Ametoa kauli hiyo jana
jioni (Jumapili, Desemba 20, 2015) wakati akizungumza na mamia ya
wananchi waliofika kumsikiliza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika
kwenye uwanja wa mikutano wa Likangala wilayani Ruangwa, mkoani Lindi.
“Sina kinyongo na mtu
yeyote na roho yangu iko huru, hivi ndiyo nilivyo. Nilikwishatangaza
msamaha kwa hiyo ninawaomba wale niliowakwaza nao pia wanisamehe… lakini
ninawasihi kuwa milango iko wazi, wawe huru kurudi wakati wowote,”
alisema huku akishangiliwa na wananchi hao.
“Ninawataka twende
pamoja ili tulete maendeleo ya Ruangwa, huku nikisisitiza kaulimbinu
yangu ya kampeni kwamba Ruangwa kwa Maendeleo Inawezekana. Wao warudi
tu, nitawahudumia wote bila kujali itikadi zao.”
Aliwaeleza wakazi hao
wa Ruangwa na vitongoji vyake kwamba amekuja kuwashukuru kwa kumchagua
na kumpa kura nyingi la sivyo asingefanikiwa kuwa mbunge wao. “Kikubwa
ninamshukuru Mungu aliyemuongoza Mheshimiwa Rais pamoja na Makamu wake
hadi wakanipa jukumu hili,” alisema.
“Kipekee ninamshukuru
Mungu aliyemuongoza Mheshimiwa Rais na kutupa sisi wana Ruangwa
tusaidiane kulibeba jukumu hili. Ninawahakikishia kuwa pamoja na jukumu
hili la kitaifa, sitawaacha wala sitawaangusha. Nitakwenda mikoa mingine
hapa nchini ili kuwasikiliza na kuwahudumia Watanzania huku nikijua
kwamba mpo salama,” alisema.
Aliwaeleza wananchi hao
kwamba bila kujali itikadi za vyama, ameunda timu ya madiwani 22 kutoka
kata zote za jimbo hilo ambayo atafanya nayo kazi kwa karibu ili
kuhakikisha matarajio ya wana-Ruangwa yanatimia. Madiwani wanane kati
hao 22 wanatoka UKAWA na 14 wanatoka Chama cha Mapinduzi (CCM).
Akigusia mipango ya
maendeleo kwa jimbo hilo, Waziri Mkuu alisema ameamua kuweka umeme wa
nishati ya jua kwenye shule zote na zahanati zote ambazo hazitafikiwa na
umeme wa gridi ya Taifa kwa sababu ziko pembezoni mwa jimbo hilo.
“Nafanya hivi kwa
sababu sipendi watoto wetu wakose masomo ya jioni kwa sababu ya kukosa
umeme au washindwe kufanya mafunzo kwa vitendo (practicals) kwa vile
wamekosa umeme,” alisema.
Mapema, akiwa njiani
kuelekea Ruangwa, Waziri Mkuu alisimama kwa muda kijijini kwao Nandagala
katika kata ya Mnacho, na kuwasalimia wananchi waliojitokeza kumpokea
kwa nderemo na hoihoi kibao.
Katika mkutano wa
hadhara ulioandaliwa kijijini hapo, Waziri Mkuu alikabidhiwa zawadi
mbalimbali yakiwemo mavazi ya kimila pamoja na silaha za jadi.
Aliwataka wakazi hao
wamvumilie kwa sababu ratiba sasa itabadilika na hawatamuona mara kwa
mara kama ilivyokuwa awali kwa vile anapaswa awahudumie Watanzania wote.
“Zile safari za jimboni zitapungua sana lakini mjue ni kwa sababu niko
kwa ajili ya Watanzania wote wa nchi hii,” alisema.
0 comments :
Post a Comment