Dar es salaam
SERIKALI kupitia Wizara ya Afya
na Ustawi wa Jamii imetenga kiasi cha Tsh. Bilioni 5 katika mwaka
2015/16 kwa ajili ya kuhudumia kambi za Madaktari Bingwa wa Magonjwa ya
Moyo ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za matibabu ya magonjwa hayo
kwa Watanzania.
Lengo la mkakati huo ni
kuhakikisha Wagonjwa wengi wanahudumiwa katika kipindi kifupi pamoja na
kupunguza gharama za kusafirisha wagonjwa nje ya nchi, ambao wengi wao
husafiri kwa ajili ya matibabu ya magonjwa ya moyo, figo na saratani.
Akizungumza na Waandishi wa
Habari leo Jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi
wa Jamii, Dkt. Donald Mmbando wakati wa ziara yake ya kutembelea
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete iliyopo katika Hospitali ya Taifa
Muhimbili.
Dkt. Mbando alisema katika wiki
ya kwanza iliyoanza wiki hii Madaktari hao wanatarajia kutoa huduma kwa
wagonjwa 20 na kuifanya Serikali kuokoa kiasi cha Tsh. Milioni 500
ambazo zingetumika kuwasafirisha wagonjwa hao nje ya nchi kwa ajili ya
matibabu.
“Tumeokoa kiasi cha Tsh. Bilioni
1 zilizopaswa kutumika kuwapeleka nje ya nchi wagonjwa hawa,
tutahakikisha kuwa Wataalamu hawa wanafanya kazi kwa pamoja na Madaktari
wetu ili waweze kuwajengea uwezo katika kutibu magonjwa haya” alisema
Dkt. Mmando.
Alisema Serikali pia ipo katika
mchakato wa kuzijengea uwezo hospitali mbalimbali nchini ikiwemo Taasisi
ya Kansa ya Ocean Road na Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) kwa
kuziwezesha hospitali hizo kuwa na Wataalamu na majengo ya kisasa kwa
ajili ya kutoa huduma za matibabu kwa Watanzania.
Aidha alisema Serikali imepanga
kufanya mazungumzo na taasisi za kiraia na nyingine ikiwemo taasisi ya
Rotary Club zilizokuwa zikisafarisha watoto wenye matatizo ya ugonjwa wa
moyo, kuwekeza nguvu nchini kwani Tanzania kwa sasa ina wataalamu wa
kutosha kwa ajili ya kuwatibu wagonja hao.
Kwa mujibu wa Mmbando alisema
magonjwa ya moyo ni miongoni mwa magonjwa yasiyoambukiza, hivyo
aliwataka Watanzania kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi mara kwa mara
na kuacha kunywa pombe na uvutaji wa sigara na kutazama desturi za
ulaji.
Kwa upande wake Mkuu wa Taasisi
ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Prof. Mohammed Janabi alisema katika kipindi
cha wiki mbili ambazo madaktari hao watakuwepo hapa nchini wanaweza
kuhudumia jumla ya wagonjwa 55, na hivyo kuifanya Serikali kuokoa kiasi
cha Tsh. Bilioni 1.2


0 comments :
Post a Comment