@nkupamah on December 2, 2015
……………………………………………………………………………………………
Na Anna Nkinda – Maelezo
Watanzania wametakiwa kutumia
technolojia ya mawasiliano ikiwemo kufanya mikutano kwa njia ya video
ambayo itawaondolea gharama ya kusafiri na hivyo kuokoa fedha na muda.
Rai hiyo imetolea hivi karibuni
na Mkurugenzi Mtendaji wa TaGLA Charles Senkondo wakati akiongea na
waandishi wa habari wakati wa mkutano wa kazi wa video conference kati
ya Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Taasisi zake,
Sekretarieti za mikoa na Mamlaka za Serikali za mitaa.
Senkondo alisema kufanya mikutano
kwa njia ya video kunamfanya mtu asisafiri na hivyo kuepukana na ajali,
kutopoteza muda awapo safarini na na kupata wasaa wa kukaa na familia
yake.
“Kuanzishwa kwa TaGLA kumeongeza
uwezo wa kufanya kazi kwa ubunifu zaidi, kwa njia ya kisasa, kwa maamuzi
zaidi ya kiuendeshaji kwa kuangalia kila mara mahitaji ya wadau na
kutumia mbinu za soko katika utoaji wa huduma bora”.
“Kabla ya kukuwa kwa teknolojia
watu walikuwa wanasafiri umbali mrefu kwenda kushiriki mikutano hivi
sasa wamepunguza safari zisizo na umuhimu. Mtu atasafiri katika
mikutano ya umuhimu tu zamani ilikuwa lazima mtu aje sasa hivi anafuatwa
popote alipo na kuletwa katika video conference”, alisema Senkoro.
Akiongelea kuhusu kituo hicho
Mkurugenzi huyo alisema zaidi ya washiriki elfu 20 wameshiriki midaharo
na mafunzo 783 ya kubadilishana maarifa kupitia Wakala wa Mafunzo kwa
njia ya Mtandao (TaGLA) .
Senkondo alisema wakala hiyo
imeweza kutoa mafunzo kwa viongozi wakiwemo mawaziri, wakuu wa taasisi
mbalimbali za umma na binafsi na kuleta urahisi wa vikundi na watu
waliotengwa kijiografia kuonana, kusikilizana na kukubaliana kwa wakati
mmoja.
“Wakala kwa kushirikiana na Ofisi
ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa kutumia mitandao ya
teknolojia imeweza kufundisha watendaji wakuu wa Taasisi za Serikali,
wakurugenzi wa Halmashauri za wilaya zote na wakurugenzi wa rasilimali
watu wapatao 1,200 mfumo wa malipo ya mishahara kwa watumishi wa
Serikali (HCMIS) Lawson version 7”, alisema Senkoro.
Mkurugenzi huyo mtendaji
alizitaja changamoto wanazokabiliana nazo kuwa ni fikra potofu juu ya
matumizi ya TEHAMA na kukubalika kwa kasi kwa teknolojia na kuwaomba
waandishi wa habari pamoja na wadau wengine kuelimisha wananchi kuhusu
umuhimu wa matumizi ya Tehama.
Senkoro alisisitiza, “Tunawaalika
wadau mbalimbali wakiwemo taasisi za Serikali na zisizo za kiserikali,
waandishi wa habari, watu binafsi na asasi za jamii watumie huduma zetu
ambazo tunazitoa kwa gharama naafuu kuweza kuwafikia wadau wengi kwa
muda mfupi bila kujali umbali au changamoto za kijiografia.
Wakala wa Mafunzo kwa njia ya
Mtandao umewezesha kufanyika kwa mahakama kwa kutumia mikutano ya video
katika kesi mbalimbali kwa kutoa ushahidi wake kwa njia ya video na
kusaidia kupunguza gharama na kuhamasisha maamuzi na hivyo utoaji wa
haki katika kesi husika.
Mkutano huo wa kazi wa video
conference kati ya Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Taasisi zake, Sekretarieti za mikoa na Mamlaka za Serikali za mitaa
ulijumuisha viongozi wa Serikali kutoka mikoa ya Dodoma, Lindi, Geita,
Singida, Pwani, Mara, Iringa, Mtwara, Shinyanga na Njombe.


0 comments :
Post a Comment