.Dar es Salaam.
Wavuvi
waishio ukanda wa maeneo ya Pwani ya Bahari ya Hindi upande wa Tanzania
Bara na Zanzibar wanatarajia kunufaika na elimu ya ukuzaji viumbe
kwenye maji na teknolojia sahihi ya kupambana na mabadiliko ya tabia
nchi kupitia mradi wa Udhibiti wa Uvuvi na Maendeleo Shirikishi Kusini
Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFISH).
Hayo
yamesemwa jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Msaidizi kutoka Idara ya
Maendeleo ya Uvuvi, Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi Bi. Fatma
Sobo alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa
mradi wa Udhibiti Uvuvi na Maendeleo Shirikishi Kusini Magharibi mwa
Bahari ya Hindi, ulioanza kutekelezwa mwezi Juni mwaka huu.
Amesema lengo
la mradi huo ni kuwasaidia wavuvi wadogo wa ukanda huo ili waweze
kunufaika na shughuli hiyo na kuwa na uvuvi endelevu wenye kuongeza
faida kiuchumi, kijamii na kimazingira.
‘Lengo la
mradi huu ni kuhakikisha kuwa wavuvi wa ukanda wa Pwani wanakuwa na
uvuvi endelevu na wananufaika na rasilimali za bahari kwa kuimarisha
uwezo wa Taasisi za Kikanda na Serikali” Amesema.
Ameeleza
kuwa katika kufuatilia utekelezaji wa mradi huo , Wizara ya Maendeleo
ya Mifugo na Uvuvi,imeanzisha mpango wa uongozi na usimamizi wa uvuvi
ambapo wavuvi wanapatiwa elimu kuhusu aina za samaki, aina ya nyavu za
kuvulia, muda wa kuvua, mauzo na uhifadhi wa samaki.
Ameongeza
kuwa mradi huo utaimarisha mfumo wa taarifa za uvuvi kama vile mavuno,
nguvu ya uvuvi inayotumika , mauzo ya ndani na nje nchi yatokanayo na
shughuli hizo.
Bi. Fatma
aliongeza kuwa kipaumbele cha mradi huo kimewekwa katika uvuvi wa samaki
aina ya pelagiska, Jodari, Kamba miti, samaki mwamba, pweza na ukuzaji
viumbe kwenye maji bahari ambapo eneo la majaribio litakuwa katika
wilaya za Mkinga, Pangani, Tanga, Bagamoyo mjini na Lindi Vijijini.
Aidha,
amesema mradi huu utatekelezwa kwa miaka 6, kuanzia 2015 hadi 2021 na
umefadhiliwa na Mfuko wa Mazingira Duniani na Mfuko wa Kimataifa wa
Maendeleo kwa jumla ya Dola za Kimarekani milioni 36,000 ambapo
utazihusisha wilaya 16 kutoka ukanda wa bahari ya Hindi, mkoa wa Tanga
hadi Mtwara.
Ameongeza
kuwa mradi huo ukizishirikisha Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi
(Tanzania Bara), Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Zanzibar) na Mamlaka ya
Kusimamia Bahari Kuu utakomesha uvuvi haramu wa kutumia Mabomu.
Taasisi
zitakazotelekeza mradi huo ni Wakala wa Mafunzo ya Elimu ya Uvuvi,
Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), Kitengo cha Hifadhi za
Bahari na Maeneo Tengefu, Vikundi vya Ujasiriamali na Jamii za watu wa
Pwani.
0 comments :
Post a Comment