*Apiga marufuku mahindi ya msaada kutengenezea pombe
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amepiga marufuku chakula cha msaada kutumiwa kutengeneza pombe za
kienyeji na kwamba atakayekamatwa atachukuliwa hatua za kinidhamu.
Ametoa kauli hiyo wakati akizungumza kwa nyakati tofauti kwenye mikutano ya hadhara iliyofanyika leo (Jumatatu, Desemba 21, 2015) kwenye vijiji vya Nangurugai, Machang’anja na Narungombe katika kata za Mbwemkuru na Narungombe wilayani Ruangwa, mkoani Lindi.
Waziri Mkuu alikuwa akijibu hoja
za diwani wa Narungombe, Bw. Rashid Nakumbya aliyetoa ombi la kuongezewa
chakula cha msaada kwa sababu wana hali mbaya. Alisema msimu uliopita
haukuwa mzuri kiuzalishaji kutokana na hali mbaya ya hewa. Pia aliomba
wasaidiwe kuboreshewa huduma za maji safi na salama.
“Natambua kuwa kuna tani 2,000 za
chakula zimeletwa katika mkoa wetu lakini hizo hazitoshi kwa sababu
mahitaji yetu ni zaidi ya tani 5,000. Chakula hiki hakitoshi kwa sasa
lakini kitasaidia kupunguza makali ya njaa,” aliwaeleza wakazi hao.
“Tumepiga marufuku kutumia
chakula cha msaada kupikia pombe. Mwananchi atakayekutwa akitumia
chakula hicho, atachukuliwa hatua za kinidhamu,” alisisitiza.
Alitumia fursa hiyo
kuwahakikishia kauli ya Rais Dk. John Pombe Magufuli kwamba hakuna
mwananchi atakayekufa kwa njaa. “Mheshimiwa Rais ameahidi kuwa hakuna
Mtanzania atakayekufa kwa njaa. Tuna mahindi ya kutosha kwenye maghala
ya Songea, Dodoma na Makambako lakini changamoto ni namna ya
kuyasafirisha kutoka huko hadi kuyafikisha huku. Tunaendelea pia
kupeleka misaada kwenye mikoa mingine,” alisema Waziri Mkuu.
Akijibu hoja nyingine
zilizotolewa, Waziri Mkuu ambaye pia ni mbunge wa jimbo hilo alisema
anatambua changamoto walizonazo za ukosefu wa maji safi, ubovu wa
barabara, zahanati na nyumba za waganga na kwamba ameanza
kuzishughulikia.
“Hivi sasa nimeanza kushughulikia
suala la uwekaji wa nishati ya umeme wa jua kwenye shule za msingi na
zahanati. Mtaalam ameshafika hapa wilayani kwetu na ameanza hiyo kazi,
na hivi karibuni mtamuona akifika maeneo ya huku,” alisema.
Kuhusu maji safi na salama,
Waziri Mkuu aliwaeleza wakazi hao kwamba tatizo la maji analijua na
kwamba changamoto kubwa waliyonayo ni upatikanaji wa chanzo cha maji
baridi kwani kiasi kikubwa eneo hilo lina vyanzo vya maji yenye chumvi.
“Wataalamu wanakuja kutafuta chanzo cha maji baridi kwa sababu asilimia
kubwa ya eneo hili maji yake yana chumvi,” alisema.
Aliwataka wakazi hao waendelee
kuwaombea yeye pamoja na Rais Magufuli na Makamu wake, Samia Suluhu
Hassan ili waweze kutimiza malengo waliyoahidi kwa Watanzania wakati wa
kampeni.
0 comments :
Post a Comment