Mbunge
wa Ubungo, Saed Kubenea (CHADEMA) amesema anatarajia kufufua hoja ya
kujadiliwa upya kwa ripoti ya fedha zilizokwapuliwa za Tegeta Escrow
zaidi ya Sh bilioni 200.
Akizungumza
jana alisema sababu za kutaka mjadala huo kurejeshwa ni kutaka kujua
iwapo fedha hizo ni za umma au ni mali ya Kampuni ya Independent Power
Tanzania Limited (IPTL).
Sababu nyingine aliyoitaja Kubenea ni kutaka kuchukuliwa hatua kwa wahusika wa sakata hilo, ili iwe fundisho kwa watu wengine.
Iliyokuwa
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) katika Bunge la 10,
iliwasilisha bungeni mapendezo zaidi ya 10 likiwemo azimio namba moja la
kuitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na
Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), kumkamata Mkurugenzi Mkuu wa
Kampuni ya Pan Africa Power Ltd (PAP) Harbinder Singh Sethi na
kumfikisha mahakamani kwa makosa ya utakatishaji wa fedha na ukwepaji
kodi.
Kamati
inaelekeza Serikali kutumia sheria za nchi, ikiwamo sheria ya Proceeds
of Crime Act, kuhakikisha kuwa Singh Sethi anarejesha fedha zote
alizochota kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Kwa mujibu wa Taarifa ya CAG iliyothibitishwa na TAKUKURU, fedha hizo pia ziligawiwa kwa watu binafsi.
Aliyekuwa
Mwenyekiti wa Kamati ya PAC, Zitto Kabwe, alisema kamati yake
ilijiridhisha kuwa fedha iliyotumika kulipia manunuzi hayo ni fedha
ambayo sehemu yake ni ya umma iliyochotwa bila huruma wala aibu, kutoka
Benki Kuu (BoT).
Akaunti hiyo ilifunguliwa na Serikali kwa pamoja kati ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Kampuni ya IPTL.
Fedha
hizo zilizua mjadala mkubwa bungeni, ambapo Rais mstaafu Jakaya Kikwete
aliweka msimamo wa Serikali kupitia mkutano wa wazee wa Mkoa wa Dar es
Salaam, akisema kuwa fedha hizo hazikuwa za umma na hivyo kuzidisha
mjadala.



0 comments :
Post a Comment