NKUPAMAH MEDIA :
Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Bw. Ramadhan Kailima alipozindua kituo Cham mawasiliano ambapo Jumla ya Simu 1,381 zilipokelewa katika kituo cha Mawasiliano cha Tume ya Taifa ya Uchaguzi – Nec Call Center, kilichoanzishwa mahususi kwa lengo la kuwasaidia wapiga kura pamoja na wadau mbalimbali wa uchaguzi ili kupata elimu ya mpiga kura
.
……………………………………………………………………………………………………………..…..
Na Lydia Churi-NEC
Hivi karibuni, Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kushirikiana na Mradi wa ukuzaji wa Demokrasia nchini (DEP) chini ya shirika la Maendeleo la Kimataifa (UNDP) iliandaa mikutano ya tathmini ya utoaji wa Elimu ya Mpiga Kura wakati wa Uchaguzi Mkuu mwaka jana ili kujadiliana juu ya kuboresha utoaji wa Elimu hiyo katika Chaguzi na kuboresha ushirikiano kati ya Tume na Wadau mbalimbali wa Uchaguzi.
Mikutano hiyo pia ililenga kuainisha maeneo ambayo wadau wanataka yafanyiwe marekebisho ili kuboresha utendaji kazi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi katika kukuza Demokrasia nchini na kupunguza changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa Chaguzi.
Mikutano hiyo ilifanyika kwa Kanda kwa kuwashirikisha Mwenyekiti wa Tume na Makamishna, Mkurugenzi wa Uchaguzi Wakuu wa Idara pamoja na Maafisa Kutoka Tume ya Taifa ya uchaguzi na Mikoa iliyoalikwa kwenye Mkutano huo.
Mikutano hii ilifanyika kuanzia Februari 2 hadi 11, mwaka huu katika miji ya Manyara, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Lindi, Mtwara, Mbeya, Rukwa na Katavi. Miji mingine ni pamoja na Pwani, Dar es Salaam, Morogoro, Unguja, Pemba, Dodoma, Singida, Tabora, Kigoma, Kagera, Mwanza, Geita, Shinyanga, Mara, Simiyu, Ruvuma, Njombe na Iringa.
Aidha, Mikutano hiyo ilishirikisha wadau mbalimbali wa Uchaguzi wakiwemo wawakilishi wa Asasi za Kiraia wa makundi mbalimbali ya jamii kama vile Wanawake, Vijana, Watu wenye Ulemavu, na Wazee. Wengine ni Waratibu wa Uchaguzi wa Mikoa (Regional Election Coordinators), Wasimamizi wa Uchaguzi wa Majimbo ambao pia ni Wakurugenzi wa halmashauri (Rertuning Officers), Maafisa Uchaguzi na Maafisa Habari kutoka kila Halmashauri ulipofanyika mkutano wa wadau.
Kwa mujibu wa Ibara ya 74(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na kifungu cha 4C cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, Tume ya Taifa ya Uchaguzi, imepewa jukumu la kutoa Elimu ya Mpiga Kura na kusimamia Asasi, Makundi au watu wanaotoa Elimu hiyo.
Kwa kuzingatia umuhimu wa jukumu hilo, Tume ilishirikisha Asasi za Kiraia 447 katika kuhamasisha wananchi na kuwaelimisha juu ya umuhimu wa kushiriki na kujitokeza kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na pia kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Asasi za Kiraia ni wadau wakubwa katika mchakato wa Uchaguzi kwa kuzingatia ukweli kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi peke yake haiwezi kuwafikia Watanzania wote kutokana na kutokuwa na rasilimali watu ya kutosha katika kuwafikishia Elimu ya Mpiga Kura pamoja na utaalamu mbalimbali wa utoaji wa Elimu hasa jinsi ya kuwafikia watu wenye mahitaji maalumu kama walemavu, wanawake, vijana pamoja na wale walioko pembezoni na maeneo yasiyofikika kwa urahisi kwa sababu mbalimbali zikiwemo za miundombinu
Pamoja na kazi ya kuelimisha Umma juu ya umuhimu wa kupiga kura kufanywa na Asasi za Kiraia kwa niaba ya Tume, Tume ya uchaguzi pia inayo wajibu wa kuifanya kazi hiyo ambapo katika uchaguzi mkuu uliopita ilifanikiwa kuandaa vijitabu, Mabango ya (Karatasi, Vitambaa na Billboards) pamoja na michezo ya kuigiza na matangazo yote ambayo yalilenga kuelimisha na kuhamasisha umma umuhimu wa kujitokeza kupiga kura.
Tume pia ilishiriki katika vipindi mbalimbali vya Redio na Luninga na kutoa ufafanuzi wa baadhi ya mambo yanayohusu Uchaguzi na kuelimisha Umma.
Pamoja na hayo, Tume ilifungua kituo cha mawasiliano ambapo wananchi waliweza kupiga simu bure kwa namba hii (0800782100) ambapo waliweza kuuliza jambo lolote linalohusu Uchaguzi Mkuu pamoja na kujua kituo chao cha kupigia kura.
Kituo hiki cha mawasiliano kilikuwa cha mafanikio makubwa ambapo jumla ya simu 78,911zilipokelewa na kupatiwa majibu.
Aidha, katika mikutano ya wadau iliyofanyika mikoani hivi karibuni wadau walitoa michago yao katika kuboresha suala la utoaji wa Elimu ya Mpiga Kura katika chaguzi zijazo. Baadhi ya maoni ya wadau yalikuwa ni kuitaka Tume itumie Wakurugenzi wa Halmashauri nchini kutoa Vibali kwa Asasi za Kiraia zinatoa Elimu ya Mpiga Kura Wakati wa uchaguzi Mkuu badala ya Tume Makao Makuu kuendelea kufanya kazi hiyo.
Wadau hao pia waliitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi ifungue ofisi zake Mikoani ili kurahisisha utendaji kazi pamoja na kupunguza au kuondoa malalamiko kuwa Kura huwa zinaibiwa. Pia waliitaka Tume iangalie namna ya kuweka utaratibu mzuri utakaoziwezesha Asasi za Kiraia kuhakiki Mabango ya kutoa Elimu ya Mpiga Kura kabla ya Asasi hizo kuomba fedha kutoka Kwa wafadhili.
Utoaji wa Elimu ya Mpiga Kura kuwa endelevu badala ya Elimu hiyo kutolewa wakati wa Uchaguzi Mkuu tu ni miongozi mwa maoni yaliyotolewa na wadau wakati wa mikutano ya tathmini ya Elimu ya Mpiga kura. Aidha Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeshauriwa na Asasi za Kiraia kuwa na fungu kwa ajili ya kuzisaidia Asasi za Kiraia ziweze kutoa Elimu ya Mpiga kwa wakati kwani katika chaguzi zilizopita elimu hiyo imekuwa ikitolewa kwa muda mfupi.
Suala la ugawaji wa majimbo pia lilijitokeza kwenye mikutano ya tathmini ya Elimu ya Mpiga Kura. Asasi za Kiraia ziliishauri Tume kugawa majimbo mapema ikiwezakana kabla ya kuanza kwa mchakato wa Uchaguzi ili kuziwezesha Asasi hizo Kujua ukubwa halisi wa jimbo na namna ya kuwafikia Wapiga Kura.
Pamoja na jitihada zote za Tume katika kuhamasisha Wapiga Kura, kumekuweko na changamoto chache za uelewa kuhusu zoezi zima la Upigaji Kura na umuhimu wake.
Kukosekana kwa fedha kutoka katika vyanzo sahihi, Asasi zililazimika kutafuta kutoka kwa wafadhili mbalimbali kulikosababisha baadhi ya Asasi kufundisha mambo ambayo mfadhili anayataka.
Kutofuata Sheria, Kanuni na miongozo iliyotolewa na Tume katika uendeshaji wa zoezi la kutoa Elimu ya Mpiga Kura kulisababisha baadhi ya Asasi kuendesha zoezi hilo kinyume na maelekezo ya Tume kwa kutoa Elimu kwa misingi ya kisiasa.
Baadhi ya Asasi kutopata Fedha na nyingine kuchelewa kupata, kulisababisha baadhi ya maeneo hasa ya Vijijini kutopata Elimu na hata waliopata elimu hiyo haikuwa ya kutosha kutokana na muda kuwa mfupi wa kutoa Elimu hiyo.
Ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza wakati wa uchaguzi, Tume ya Taifa ya Uchaguzi inapaswa kuzingatia maoni na ushauri uliotolewa na Asasi za kiraia. Hata hivyo Asasi za Kiraia nazo hazina budi kuweka maslahi ya nchi mbele kwa kufuata sheria ili kuleta mshikamano na kudumisha amani na utulivu vilivyojengeka nchini kwa miaka mingi.
Tume inatarajia kuwa Asasi za Kiraia zitaendelea kutoa ushirikiano na kufanya kazi kwa pamoja ili kuendeleza utoaji wa Elimu kwa watanzania na hatimaye kukuza Demokrasia nchini pia kuwaelimisha wananchi juu ya haki na wajibu wao katika michakato mbalimbali ya Chaguzi ikiwemo uandikishaji wa Wapiga Kura, Uchaguzi wenyewe na hata katika Kura za Maoni.


0 comments :
Post a Comment