Nkupamah media:
Wakizungumza kwa nyakati tofauti mjini hapa jana, walimu hao walisema mpaka sasa hawajui ni lini serikali itawalipa stahiki zao ambazo ni posho za usimamizi wa mtihani huo.
Kwa taarifa zilizopatikana walimu ambao hawajalipwa fedha hizo ni kutoka halmashauri za Kilosa, mkoani Morogoro na Manispaa ya Dodoma.
Kwa mujibu wa mmoja wa walimu hao ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, walilipwa malipo nusu, huku wakiahidiwa kulipwa mapema kiasi kilichobaki lakini hadi sasa haykijatolewa.
"Yaani hadi matokeo ya mitihani yametoka sisi bado hatujalipwa fedha zetu za usimamizi," alisema mwalimu huyo.
Hivi karibuni katika kikao cha wakuu wa shule za sekondari Manispaa ya Dodoma, Mwenyekiti wa Chama cha Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari Tanzania (Tahosa), Richard Kileo, alisema walimu hao wamekuwa wakipigwa danadana za malipo hayo bila kuambiwa lini watalipwa.
"Serikali iliangalie suala hili kwani linawakatisha tamaa watu ambao wanatumia muda mwingi kuitumikia nchi yao lakini malipo yao yamekuwa na kigugumizi," alisema Kileo.
Hata hivyo, katika mkutano wa pili wa Bunge la 11, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Joyce Ndalichako, alisema wizara hiyo haihusiki na madai hayo, Tamisemi na idara zake.
Akizungumzia madai hao katika kikao na watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma, Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi na Utawala Bora, Seleman Jafo, alikiri baadhi ya walimu hawajalipwa posho hizo, huku akisema Tamisemi inaendelea na jitihada za kuhakikisha fedha zinapatikana ili waweze kulipwa.
"Kuna tatizo walimu ambao waliosimamia mitihani ya kidato cha nne mwaka jana wengine hawajapata fedha zao kutokana na maombi yaliyopelekwa na Tamisemi katika Ofisi ya hazina lakini fedha zilizokuja kulikuwa na upungufu wa Sh. bilioni nne," alisema Jaffo.
Alisema kutokana na fedha hiyo kupungua ndio maana kuna watu hawajalipwa lakini Tamisemi imewaagiza watendaji wake wafuatilie fedha hizo Hazina ili walimu hao walipwe.


0 comments :
Post a Comment