Nkupamah media:
NA VICTOR MASANGU, KISARAWE PWANI
NAIBU Waziri Ofisi ya Rais
Tamisemi Utumishi na Utawala bora, Seleman Jafo amemuagiza Mkurugenzi
wa Halmashauri ya wilaya ya Kisarawe kumtafutia kazi nyingine meneja wa
Mamlaka ya Bodi ya Maji Kisarawe Listern Materu kutokana na kushindwa
kutatua kero ya maji kwa muda mrefu.
Jafo ambae pia ni mbunge wa
jimbo la Kisarawe alisema, hawawezi kuendelea kukaa na watumishi ambao
hawaguswi na matatizo ya wananchi.
Alitoa agizo hilo juzi mjini
Kisarawe, kwenye mkutano aliouandaa kwa ajili ya kuwashukuru wananchi
kwa kumpa ridhaa ya kuendelea kuongoza jimbo hilo, na kusikiliza kero
zinazowakabili wananchi hao.
Naibu Waziri huyo alimtaka
Materu kuachia nafasi ya Meneja ili apangiwe kazi nyingine kwani
ameshindwa kutatua changamoto ya maji katika mji wa Kisarawe.
“Mkurugenzi mtafutie kazi
nyingine katika ofisi yako, hatuwezi kuwa na watu ambao hawaguswi na
matatizo ya watu tafuta atakayekaimu nafasi yake katika kipindi hiki.
Hatufanyi mambo ya kuchekeana,
na hatuwezi kuibadilisha Kisarawe yetu kama tutaendelea kuwavumili
watumishi wanaochangia kudumaza maendeleo”alisema Jafo.
Inadaiwa kuwa, Materu amekua
meneja wa Mamlaka hiyo kwa zaidi ya miaka kumi lakini hakuna njia
mbadala iliyobuniwa na mamlaka hiyo kuondoa tatizo la maji kukosekana
mara kwa mara.
Mji huo wa Kisarawe una chanzo
cha maji cha kimani ambacho kinatoa lita 16000 kwa saa na chanzo kingine
cha minaki kinachotoa zaid ya lita 10,000 kwa saa hali ambayo ni
dhahiri kusingekuwepo na tatizo la maji.
Wananchi waliohudhuria katika
mkutano huo walifurahishwa na kitendo kilichofanywa na mbunge wao huku
wakiendelea kumuomba ahamie katika idara ya ardhi.
Mwajuma Yusuph, Salehe Ally na
Said Issa walisema kitendo cha kuondolewa Meneja huyo kitaleta
mabadiliko kwani baadhi ya watumishi wanafanya kazi kwa mazoea bila
kujali adha inayowapata wananchi.
0 comments :
Post a Comment