Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Balozi wa Japan nchini, Masaharu
Yoshida kuhusu namna ambavyo Japan inaweza kusaidia waathika wa
tetemeko la ardhi mkoani Kagera. Mazungumzo yao yalifanyika Ofisini kwa
Waziri Mkuu jijini Dares salaam Septemba 19, 2016. Kulia ni Mwakilishi
Mkuu wa JICA nchini, Toshio Nagase.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa
amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Japani nchini, Mheshimiwa
Masaharu Yoshinda ambaye amemueleza kwamba Serikali yake ipo tayari
kukarabati shule zilizoharibiwa na tetemeko la ardhi lililotokea mkoani
Kagera.
Pia imeomba kupatiwa orodha ya
mahitaji ya dharura yakiwemo mahema, mablanketi, dawa na vifaa tiba kwa
ajili ya kuwasaidia waathirika wa tetemeko hilo.
Balozi Yoshinda ameyasema hayo leo
(Jumatatu, Septemba 19, 2016) wakati alipokutana na Waziri Mkuu ofisini
kwake Magogoni Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuzungumzia masuala ya
maafa yalitokea Kagera.
Kwa upande wake Waziri Mkuu
ameishukuru Serikali ya Japani kwa hatua hiyo na kukiagiza Kitengo cha
Maafa kilicho chini ya Ofisi yake kuwasiliana na Ubalozi wa Japan nchini
na kuwasilisha orodha ya shule zilizoharibika pamoja na mahitaji ya
dharura.
Wakati huo huo Waziri Mkuu
amepokea msaada wa tani 2.5 za mchele, magodoro 200, mablanketi 100 na
fedha taslimu sh. milioni 10 ili kusaidia wananchi waliothirika na
tetemeko hilo.
Msaada huo umetolewa na wadau
mbalimbali akiwemo Ofisa Utumishi wa Kampuni ya Chang Qing Inernational
Investiment Limited ya nchini, Bi. Anna Jiang aliyetoa magodoro 200
yenye thamani ya sh. milioni sita.
Wengine ni Mkuu wa Kitengo cha
Fedha wa Benki ya Exim, George Shumbusho aliyetooa sh. milioni 10 pamoja
na Katibu Mkuu wa Chama cha Urafiki kati ya Serikali ya Tanzania na
China, Bw. Joseph Kahama aliyetoa mchele tani 2.5 pamoja na mabllanketi
100 vyote vikiwa na thamani y ash. milioni 10.
Waziri Mkuu amewashukuru kwa
misaada hiyo na kuwaomba wananchi wengine wajitokeze kwa wingi ili
kuwasaidia watu walioathirika na tetemeko hilo ambalo ni kubwa na
halijawahi kutokea nchini.
Tetemeko hilo lilitokea Jumamosi,
Septemba 10, 2016 na kusababisha vifo vya watu 17 na wengine 440
walijeruhiwa kati yao watu 253 walifikishwa Hospitali ya Mkoa, 153
walilazwa, 113 wametibiwa na kuruhusiwa na wengine 38 wanaendelea na
matibabu ambapo kati yao watu 23 wamefanyiwa upasuaji mkubwa na
wanaendelea vizuri.
Pia tetemeko hilo limesababisha
nyumba 2,063 kuanguka huku nyingine 14,081 zikiwa katika hali hatarishi
baada ya kupata nyufa na 9,471 zimepata uharibifu mdogo huku wananchi
126,315 wakiiitaji misaada mbalimbali.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
- L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM.
JUMATATU, SEPTEMBA 19, 2016


0 comments :
Post a Comment