Hatimaye
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru) imeanza
kuichunguza akaunti ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kama
ilivyoagizwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape
Nnauye katika taarifa yake iliyotolewa hivi karibuni ili kubaini madudu
yanayofanyika.
Aidha,
Nape aliamua kufikia maamuzi hayo kufuatia kupewa taarifa kupitia kwa
wadau mbalimbali kutakiwa kuichunguza akaunti hiyo ya TFF jambo ambalo
aliamua kulifanyia kazi kwa kuiagiza Takukuru kuanza kazi yake ikiwa ni
pamoja na kufuatilia chaguzi mbalimbali zinazoendelea kufanyika hivi
sasa mikoani hadi itakapofika ngazi ya TFF katika uchaguzi mkuu wa rais
utakaofanyika hapo mwakani.
Ofisa
Habari wa Takukuru, Mussa Msalaba, ameibuka na kusema kuwa, tayari
wameshaanza kutekeleza agizo hilo la Waziri Nape, ambapo wameanza
kufanya uchunguzi TFF kimyakimya.
“Tayari
tumeshaanza kufanya uchunguzi wetu wa awali na tumeanza kwa kuchunguza
akaunti za TFF pamoja na masuala mbalimbali yanayohusu shirikisho hilo,
japokuwa tunafanya kimyakimya na kwa upande wetu wenyewe tunajua
tunafanyaje kazi yetu, siyo lazima kwa upande wao wafahamu nini
kinaendelea na tunachokihitaji sisi ni kubaini kilekile tulichotakiwa
kufanya.
“Tumeanza
kazi hiyo katika mikoa yote kwenye chaguzi za mikoa na wilaya
zinazofanyika hivi sasa lakini tunakutana na ugumu wa hali ya juu kwa
kuwa suala hili watu huwa wanapeana vichochoroni au chooni lakini sisi
kama Takukuru hatutashindwa kitu na tunaendelea kufanya kazi yetu kama
tulivyopangiwa.
“Na
kwa upande wa suala la Rais wa Simba, Evans Aveva, bado mchakato
unaendelea kwa kufanya uchunguzi kwa kuwa suala lao ni pana, hivyo
linahitaji muda zaidi kabla ya kuliweka wazi,” alisema Msalaba.


0 comments :
Post a Comment