WAKATI Simba ikiwa imesaliwa na mechi sita kabla ya kumaliza msimu wa Ligi Kuu Bara, klabu hiyo imeanza kuumiza vichwa kufuatia majembe yake matatu kugoma kusaini mkataba mpya. Majembe hayo ambayo yanategemewa katika kikosi cha kwanza, mikataba yao inafikia tamati mwishoni mwa msimu huu
ambapo kwa sasa viongozi wanahaha kuhakikisha wanawabakisha kikosini hapo kwa misimu mingine ijayo. Wachezaji hao ni Ibrahim Ajibu, Jonas Mkude na Abdi Banda ambapo imeelezwa kuwa viongozi wamepata ahueni kidogo kwa Banda ambaye kwa sasa ndiye wapo naye kwenye mazungumzo ya kumpa mkataba.
Akizungumza Ijumaa, bosi mmoja kutoka ndani ya Simba ambaye hakutaka kuweka wazi jina lake, alisema wachezaji hao pekee ndiyo mikataba yao inafikia tamati mwishoni mwa msimu huu lakini bado hawajaonyesha dalili za kuongeza. “Hadi sasa wachezaji ambao wanatarajia kumaliza mikataba yao hapa Simba ni watatu tu ambao ni Banda, Mkude na Ajibu, lakini wote waliobakia wapo vizuri kwa kuwa mikataba yao ni ya muda mrefu.
“Kwa upande wa Mkude na Ajibu wenyewe tayari walishagoma kuongeza mkataba kuendelea kubaki Simba licha ya uongozi kuwafuatilia, hivyo tumeamua kuwaacha hadi hapo mikataba yao itakapoisha na kujua nini cha kufanya, lakini Banda mazungumzo yanaendelea na huenda akaongeza mkataba mwingine,” alisema bosi huyo.
0 comments :
Post a Comment