YANGA wamesikia baadhi ya mashabiki wakidai kuwa, watapoteza mchezo wao wa leo dhidi ya Azam kutokana na kukabiliwa na majeruhi ya baadhi ya wachezaji wao muhimu, lakini Wanajangwani hao wameibuka na kudai kuwa watawashangaza wote wenye mawazo hayo.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, watakuwa na kibarua kigumu mbele ya Azam FC, mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, utakaochezwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Kinachowafanya baadhi ya mashabiki na hata baadhi ya wachambuzi wa soka kudhani kuwa upepo unaweza kuwaendea kombo Yanga, ni kutokana na kukosekana kwa nyota wao, Donald Ngoma pamoja na Amis Tambwe, kutokana na majeraha yanayowakabili.
Hata hivyo, wakati Yanga wakiwakosa wakali hao, kwa upande wao Azam FC, watamkosa nahodha wao, John Bocco, kutokana na majeraha, kitu ambacho pia baadhi ya mashabiki wametilia shaka kuwa huenda pengo lake likawaathiri wanalambalamba hao kutokana na umuhimu wake.
Licha ya kwamba Yanga watawakosa wachezaji wao hao, lakini wanaamini kuwa, ushindi ni lazima, kwani kikosi chao hakitegemei mchezaji mmoja, huku Azam nao wakichimba mkwara kuwa, licha ya kwamba watamkosa Bocco, watazoa pointi tatu muhimu.
Kocha msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi, ameweka wazi kuwa, licha ya kwamba mchezo huo utakuwa mgumu kutokana na historia ya upinzani timu hizo zinapokutana, wanachokiangalia ni kuhakikisha wanafanya vizuri.
“Ni mchezo mgumu, kwani wapinzani wetu nao wanajulikana ubora wao, ila yote kwa yote, kwa upande wetu tumejiandaa vizuri na tunachosubiri ni dakika 90 kumalizika ndipo tutakapojua nani mbabe,” alisema.
Kwa upande wake, Kocha Msaidizi wa Azam FC, Idd Cheche, alisema: “Ni mchezo mgumu sana, lakini hatulazi macho, kwani hii Ligi yetu kila mmoja anamjua mwenzake, ninachoweza kusema ni kwamba, tumejiandaa vizuri na tunataka kuondoka na pointi tatu.”
Mchezo huo unatarajiwa kuwa mgumu, kutokana na hali halisi ya mbio za ubingwa, hasa kwa timu kongwe, Simba na Yanga, ambapo Wanajangwani hao wanajua kuwa wakipoteza watajitengenezea mazingira magumu ya kutetea ubingwa wao.
Katika msimamo wa Ligi hiyo, Simba ndio wanaoongoza wakiwa na jumla ya pointi 55, Yanga wakifuatia katika nafasi ya pili wakiwa na pointi 53 na Azam FC, wakiwa na pointi 44, kila moja ikiwa imecheza michezo 24.
Katika mchezo huo, Yanga wanajua kuwa wapinzani wao, Simba, wamejipanga kuhakikisha wanaharibu sherehe yao leo ili wazidi kuwaacha kwenye mbio za ubingwa, kitu ambacho Wanajangwani hao wamekishtukia na sasa wamejipanga kukwepa hujuma za aina yoyote.
Mchezo huo utachezeshwa na mwamuzi pekee wa kike nchini aliyeteuliwa kuchezesha fainali za michuano ya Kombe la Dunia kwa wanawake mwaka 2019, zitakazofanyika nchini Ufaransa, Jonesia Rukyaa.
Jonesia ni miongoni mwa waamuzi waliochaguliwa hivi karibuni kutoka Afrika kushiriki katika mafunzo na mitihani ya kuchezesha michuano hiyo ya Kombe la Dunia na endapo atafanya vizuri katika mitihani hiyo, iliyofanyika Ureno, atapangwa kwenye ratiba.
Pia mwanadada huyo amewahi kuchezesha michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wanawake, iliyofanyika Cameroon mwaka jana na kuwa mwamuzi wa kwanza wa kike nchini kuchezesha michuano hiyo mikubwa barani Afrika.
About Unknown
This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.