Mwanasheria mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Tundu Lissu amerudishwa tena rumande baada ya mahakama ya hakimu mkazi Kisutu kusema itatoa uamuzi juu ya maombi ya dhamana yaliyowasilishwa na mawakili wake Alhamis wiki hii.
Lissu amerudishwa rumande baada kukamatwa siku ya Alhamis wiki iliyopita akiwa chini ya uangalizi wa jeshi la polisi kanda maalumu ya Dar es Salaam na jana amesomewa shtaka moja linalohusu kutoa kauli za uchochezi.
Upande wa jamhuri uliwakilishwa na jopo la mawakili wanne wakiongozwa na wakili Mutalemwa Kishenyi huku upande wa utetezi ukiwakilishwa na jopo la mawakili 18 wakiongozwa na Fatma Karume pamoja na Peter Kibatala chini ya hakimu mkazi mkuu wa mahakama hiyo Wilbard Mashauri.
Baada ya kusomewa shtaka hilo ndipo upande wa utetezi uliwasilisha maombi ya dhamana ambapo hata hivyo upande wa jamhuri uliiomba mahakama kutompatia mshtakiwa huyo dhamana kutokana na upelelezi kutokamilika na kwamba mshtakiwa anakabiliwa na mashtaka mengine kadhaa ambayo yote yanahusiana na kutoa kauli za uchochezi.


0 comments :
Post a Comment