Serikali ya Tanzania imefikia makubaliano na watu wa China kufanya ukarabati wa uwanja wa Taifa uliopo Temeke jijini Dar es Salaam, zoezi ambalo litagharimu kiasi shilingi bilioni 6.
Akizungumza baada ya kutiliana saini makubaliano hayo, Katibu mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dotto James amesema ukarabati huo ni msaada na siyo mkopo na lengo ni kuurejesha katika hali yake ya awali.
“Mtakumbuka uwanja huu walitusaidia pia kuujenga, huu na wenyewe ni msaada na siyo mkopo, na wataleta watu wao, kwa ajili ya ku-mantain, na kuongozea vifaa na teknolojia ya kisasa zaidi,”amesema Dotto.
Kwa upande wake kaimu balozi wa China nchini Tanzania, Gou Gaodo amesema wameona ni muhimu kuufanyia marekebisho uwanja huo kutokana na matumizi yake katika matukio makubwa ya kimichezo na kijamii.
“Kwa wakati ule huu ulikuwa ndiyo uwanja mkubwa barani Afrika, kwahiyo ili kuhakikisha unatumika vyema, serikali ya China imeamua kuuboresha. Kwa vijana uwanja ni kitu muhimu sana kwa michezo na matukio mengine makubwa,” amesema balozi huyo.
Ujenzi wa uwanja huo ulikamilika mwaka 2007 na sasa ikiwa ni miaka 10 baadaye uwanja huo unafanyiwa marekebisho kwa mara ya kwanza