Akizungumza katika mahojiano maalum na Nipashe jijini Dar es Salaam jana, Prof. Manyele alisema msingi wa kufanyika kwa kazi hiyo, unaanzia kwa Jeshi la Polisi ambalo ndilo lenye jukumu la kupeleka sampuli za mkojo kwenye ofisi zake ili kupatiwa majibu kulingana na kile wanachotaka kifanyiwe uchunguzi dhidi ya watu wanaohusishwa na matukio mbalimbali.
Prof. Manyele alisema Jeshi la Polisi hupeleka sampuli za mkojo wa mtu ambaye wanadhani hawezi kufanya tukio alilofanya kwa akili zake bali kwa sababu nyinginezo, ikiwamo matumizi ya vitu vyenye kemikali zinazoweza kuathiri matendo ya mtu.
“Mtu kafanya kitu lakini mpelelezi anaona huyu hawezi kufanya kosa hili isipokuwa akili zake haziko sawa ndiyo maana wanakuja kwetu kupata uhakika,” alisema Prof. Manyele na kuongeza:
“Kuna matukio mtu anafanya kwenye jamii (ambayo) kwa akili za kawaida hadhaniwi kushiriki kufanya hivyo. Ndiyo maana wanatilia shaka kutaka kujua nini kilisababisha kufanya hivyo. Pengine ni dawa za kulevya, mirungi au bangi na ili kupata majibu ndiyo wanaleta sampuli tuzichunguze.”
Prof. Manyele alisema ofisi yake haiwezi kuchukua sampuli za watu kuwapima isipokuwa baada ya kupata taarifa kutoka Jeshi la Polisi au kwa watu binafsi, ambao nao huwa na sababu za msingi kufanya hivyo.
“Mimi siwezi kuwapima mkojo bali naletewa sampuli za kupima. Uamuzi ni wa Jeshi la Polisi… sisi tunatekeleza uamuzi huo ili upelelezi wao uende vizuri,” alisema.
Aidha, alisema makosa madogo huwa hayasababishi mtu kupimwa mkojo isipokuwa yale yanayotiliwa shaka kwa aliyetenda tukio husika.
Alitaja baadhi ya makosa yanayosababisha mtu kupimwa mkojo kuwa ni pamoja na ubakaji, ajali na pia makosa ya jinai kama matumizi ya silaha.



0 comments :
Post a Comment