Lisu:Msajili Mutungi Asiitishe Chadema ,Ajitafakari





Barua ya msajili wa vyama vya Siasa ya kuitaka CHADEMA ijieleze ndani ya siku tano imemuinua kitandani mwansheria wa chama hicho ,Tundu Lissu ambae yupo kwenye matibabu kule nchini ubelgiji.

Tundu lissu ametumia ukurasa wake wa instagram kumjibu msajili wa vyama vya siasa kwa kuandika ujumbe ufuatao.

"MSAJILI MUTUNGI ASIITISHE CHADEMA, AJITAFAKARI  
 Nimesoma barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, yenye tuhuma na vitisho vingi dhidi ya CHADEMA. .

Bila kutoa ushahidi wowote na kwa kutegemea taarifa za upande mmoja tu, Msajili Mutungi ameituhumu CHADEMA kwa kufanya siasa za kibabe na vurugu na kukiuka Sheria ya Vyama vya Siasa na Kanuni za Maadili ya Vyama vya Siasa. .

Msajili Mutungi anastahili kujibiwa hadharani na kukumbushwa mambo kadhaa. Inaelekea amejisahau sana au anafikiria Watanzania ni wajinga wasioelewa mambo yake.
.

Msajili wa Vyama vya Siasa amekosa sifa na uadilifu (moral authority) ya kunyooshea kidole CHADEMA au chama kingine chochote cha upinzani kuhusiana na jambo lolote linahusu Sheria ya Vyama vya Siasa na kanuni zake. .

Tangu Rais John Magufuli aingie madarakani, nchi yetu imeshuhudia ukiukwaji mkubwa wa Sheria ya Vyama vya Siasa ukifanywa na Magufuli mwenyewe, mawaziri pamoja na wateule wake wengine na Jeshi la Polisi. .

Mikutano ya hadhara na maandamano ya amani, ambavyo ni haki ya vyama vya siasa kwa mujibu wa Sheria hiyo, imepigwa marufuku na Magufuli bila uhalali wowote. Msajili Mutungi hajawahi kukemea ukiukwaji huo wa sheria wala kutetea haki ya vyama vya siasa. .

Viongozi wa vyama vya upinzani, hasa CHADEMA, wameuawa, wametekwa nyara na kupotezwa, wamepigwa risasi katika majaribio ya kuuawa, wameteswa, wamekamatwa na kushtakiwa kwa kesi za uongo. .

Msajili Mutungi amekuwa bubu na kiziwi asiyesikia wala kukemea uonevu na ukandamizaji huu dhidi ya vyama anavyovisimamia. .

CCM na serikali yake zimetoa hongo kurubuni madiwani, wabunge na viongozi wengine wa vyama vya upinzani kujiuzulu nafasi zao. Yote ni makosa ya maadili kwa mujibu wa sheria. Msajili Mutungi hajawahi kuliona hilo

 Polisi wameua mwanafunzi wa chuo aliyekuwa kwenye dala dala. Wamepiga risasi za moto na kujeruhi watu wengi bila sababu yoyote ya msingi. .

Badala ya kukemea matumizi haya ya nguvu iliyopitiliza, Msajili Mutungi anaitishia CHADEMA iliyokuwa inadai haki yake ya kuwa mawakala kwenye vituo vya kura. .

Tunajua kwa nini Msajili Mutungi hajawahi kuona makosa ya watawala wakandamizaji bali anaona makosa ya wanaokandamizwa tu. .

Amefungwa macho na kuzibwa masikio na maboriti na mabanzi ya cheo chake. Ni msaka tonge anayejipendekeza kwa Magufuli ili aendelee kuwa kwenye nafasi aliyo nayo. Asitutishe. .

Kwa vile anadai tumetenda makosa ya jinai, basi asubiri Mahakama zifanye maamuzi juu ya tuhuma hizi. .

Yeye hawezi akawa mtoa tuhuma na jaji wa tuhuma hizo hizo. Nasikia amewahi kuwa Jaji wa Mahakama Kuu, anatakiwa kuyafahamu haya. .

Sasa diwani wetu huko Kilombero ameuawa kinyama. Kwa vile ni wa CHADEMA, wauaji wake ni 'watu wasiojulikana' na Msajili Mutungi na Jeshi la Polisi watafanya kama walivyofanya kuhusiana na wale waliojaribu kuniua kwa risasi lukuki September 7 ya mwaka jana: Nothing!!! Tusubiri na tuone kama Msajili Mutungi atatoa kauli yoyote kuhusu mauaji haya ya diwani wa CHADEMA. .

Katika mazingira haya ya uonevu na ukandamizaji mkubwa, ni vyema kujikumbusha maneno ya Nelson Mandela ya mwaka 1953: . "Hakuna njia rahisi ya ukombozi mahali popote, na itabidi wengi wetu tupite mara kadhaa katika bonde la uvuli wa mauti kabla hatujafikia kilele cha matarajio yetu."
.

Tangu Magufuli aingie madarakani, ametuingiza katika bonde la uvuli wa mauti. Mauaji haya na ukandamizaji huu dhidi ya vyama vya upinzani ndio bonde la uvuli wa mauti lenyewe. .

Tutalipita bonde hili mara kadhaa kabla ya kupata ukombozi wa pili wa nchi yetu. Lakini tutalivuka. Hii ndio gharama halisi ya ukombozi mahali popote na katika zama zote."
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment