…………………………………………………..
Chuo kikuu cha Binary cha nchini
Malaysia kimetoa nafasi 10 za ufadhili wa masomo ya shahada ya Uzamili
na Uzamivu katika fani za Ujasiriamali na Teknolojia ya Habari kwa
kipindi cha miaka mitatu kwa watanzania wataohitaji kusoma nchini humo.
Utiaji saini wa makubaliano ya
nafasi hizo za masomo zinazojulikana kwa jina la Binary – First Lady
of Tanzania Scholarship Award umefanyika leo katika chuo hicho kati ya
Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) Daud Nasibu
na Mwanzilishi na Mwenyekiti Mtendaji wa chuo hicho Prof. Joseph
Adaikalam na kushuhudiwa na Mke wa Rais Mhe. Mama Salma Kikwete.
Akiongea wakati wa hafla hiyo ya
utiaji saini Mke wa Rais Mhe. Mama Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa
Taasisi ya WAMA alikishukuru chuo hicho kwa kutoa nafasi 10 za masomo
ambazo zitasaidia sio tu kwa wataofaidika nazo moja kwa moja bali pia
kwa jamii ambako wahitimu watarejea kuitumikia.
Mhe. Mama Kikwete alisema kupitia
mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now) kwa upande wa elimu ya
msingi na sekondari Tanzania imelenga kujenga uwezo wa walimu kwa kutoa
mafunzo ya pahala pa kazi, kusaidia watoto wasiofanya vizuri kwa kuandaa
vitendea kazi mahsusi vinavyozingatia umri na mahitaji, kuboresha
miundo mbinu kwa kujenga madarasa, maabara na nyumba za walimu,
kuboresha vifaa vya ufundishaji kama vile madawati, vifaa vya maabara,
vitendanishi (Kemikali) na uongeza motisha kwa walimu.
“Mipango niliyotaja hapo juu
imekuwa na mafanikio makubwa kuongeza maradufu udahili wa wanafunzi
katika shule za msingi na sekondari, kuleta usawa wa kijinsia na
kupunguza kwa kiasi kikubwa upungufu wa walimu, maabara, vitabu na vifaa
vya kufundishia na kujifunzia”.
Kwa mukhtadha huo ni dhahiri kwamba fursa za Binary First Lady of Tanzania Scholarship zimekuja
kwa wakati muafaka kabisa ambapo shule zetu za sekondari na taasisi za
elimu ya juu zinatoa wahitimu wengi wanaohitaji kupata elimu za ngazi za
juu za shahada za uzamili na uzamivu. Hivyo basi narudia kuwashukuru
kwa moyo wenu wa upendo na ukarimu. Mmeifanyia nchi yetu ihsani kubwa”,
alisema Mama Kikwete.
Naye Mwanzilishi na Mwenyekiti
Mtendaji wa chuo hicho Prof. Joseph Adaikalam alisema nia ya ufadhili
huo wa masomo ni kutoa nafasi kwa wanafunzi watanzania kupata ujuzi na
utaalamu maalum ili watakapomaliza masomo yao na kurudi nyumbani waweze
kuchangia katika maendeleo ya nchi na kuwasaidia moja kwa moja
watanzania.
“Binary – First Lady Scholarships
ambayo iko chini ya mwamvuli wa Binary Global Scholarship Fund
ilianzishwa mwaka 2009 hadi sasa nafasi hizo za masomo zimeshatolewa
katika nchi za Zambia, Kenya na Senegali”.
Pia chuo kinatoa ufadhili wa
masomo kwa nchi ambazo hazina mke wa Rais ufadhili unaojulikana kwa jina
la Binary Malaysia – Bosnia Herzegovina, na Binary Malaysian –
Uzbekistan hii yote ni kuonyesha kuwa vyuo vikuu vya Malaysia
vinatambua umuhimu wa elimu”, Prof. Adaikalam.
Alisema wanafunzi wataoomba
ufadhili huo wa masomo kwa shahada ya Uzamili kiwango chao cha ufaulu
kitaanzia CGPA ya 3.5 na kuendelea na watakaokidhi vigezo wataanza
masomo mwezi wa 10 mwaka huu nchini humo.
Taasisi ya WAMA ni msimamizi wa
Binary – First Lady of Tanzania Scholarship utakaotolewa kwa kipindi
cha miaka mitatu na baada ya hapo utasainiwa tena kwa kipindi kama hicho
na kwa mwaka huu nafasi zitatolewa kwa wanafunzi wa masomo ya Uzamili.
Mwakani ufadhili utatolewa kwa wanafunzi wa Shahada ya Uzamili na
Uzamivu.


0 comments :
Post a Comment