Dar es
Salaam. Siku moja baada ya ufunguzi wa kampeni za CCM, wasomi na
wananchi wamesema kauli ya Rais mstaafu, Benjamin Mkapa kuwa wanaosema
wanataka kuikomboa Tanzania ni “wapumbavu na
malofa” haikustahili
kutolewa na kiongozi huyo.Katika ufunguzi huo, Mkapa alisema wapinzani
wanaodai vyama vyao ni vya ukombozi ni wapumbavu na malofa kwa kuwa
Watanzania walikwishakombolewa na ASP na Tanu na kwamba chama pekee cha
ukombozi kilichobaki sasa ni CCM.
Profesa
wa Uchumi katika Kilimo wa Chuo Kikuu cha Sokoine (Sua), Damian
Gabagambi alisema kauli kama hizo zinatokana na mabadiliko yanayoonekana
kwenye siasa za Tanzania yanayosababishwa na kutimia kwa unabii wa
Mwalimu Julius Nyerere kuwa ‘mpinzani wa kweli atatoka ndani ya CCM.
’Alisema
kutokana na hali hiyo, viongozi wakubwa wa CCM hawajiamini, wanalazimika
kutumia lugha zisizo na staha kupunguza msongo walionao.“Kuhama kwa
viongozi waandamizi kunawaumiza kichwa na huenda hawajui sababu.
Wameanza kampeni na matusi na pia, wamechelewa kumaliza mkutano, kwa
hali hii watatoa wapi nguvu ya kuwakemea wengine?” alihoji Profesa
Gabagambi.
Alishangazwa
na kitendo cha polisi kuendelea kutoa ulinzi bila ya kukemea baada ya
ufunguzi huo kupitiliza muda wa saa 12.00 unaoruhusiwa na akaitaka Tume
ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutoa kauli juu ya suala hilo.“Walipoteza
muda mwingi kwa burudani za wasanii, nilitarajia wangetumia muda ule
kutueleza wamefanya nini kwa muda waliokuwapo madarakani na kufafanua
walivyotekeleza ilani iliyopita.
Kwa mgeni
angeweza kudhani kuwa lilikuwa tamasha la burudani,” alisema.Mwenyekiti
wa NEC, Jaji Damian Lubuva alipoulizwa alisema: “Suala la muda
limeainishwa kwenye kanuni, navikumbusha vyama vyote vya siasa
kuzingatia maadili ya uchaguzi kwa kipindi chote cha kampeni.
Mwisho wa
kampeni ni saa 12.00 jioni na hili linapaswa kufuatwa na vyama
vyote.”Jaji Lubuva alisema vyama vyote vinatakiwa kuzingatia maadili
waliyosaini na kuzungumza mambo yanayohusu sera na ilani zao badala ya
kushambuliana na kutoleana maneno ya kuudhi majukwaani.
Katibu wa
Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alipoulizwa alisema: “Nyie
Mwananchi mkoje? Shughuli imeandaliwa na CCM, halafu mnataka CCM watoe
maoni, inawezekanaje?Hata alipofafanuliwa kuwa kauli za viongozi hao
zimehojiwa na watu mbalimbali alisema, “basi endeleeni na hao.
”Wakati
Nape akisema hayo, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM), Dk Allan Simba alisema kauli hizo ni za woga na zinataka
kuwatisha wananchi ili wasiwachague wapinzani.
Aliwataka
viongozi hao kutulia na kutoogopa kinachoendelea ili kuwapa wananchi
fursa ya kufanya uamuzi juu ya mtu wanayeridhika naye kuwatumikia.
“Kubezana
siyo haki na hatutarajii kinywa cha mzee huyu kitoe maneno makali kama
hayo ila isingeshangaza kama angeongea vile kijana yeyote kutoka ndani
ya chama. Tungejua kuwa baadaye wazee wangemuita na kumkanya ili awe
makini zaidi,” alisema.Aliongeza kuwa ni vyema ushindani ukaelekezwa
kwenye hoja ili kujenga demokrasia makini na siasa zenye weledi kwa
kuwaacha wananchi wapembue ilani za kila chama.
“Kama
upande wa pili nao watajibu kwa matusi haitashangaza kama siku moja
itatokea wakashikana mashati,” alisema.Profesa Milline Mbonile wa UDSM
alisema si jambo jema kuzingatia masuala ambayo hayakuwa lengo la
mkutano ule badala yake watu waangalie kiini ili wananchi wawe kwenye
nafasi nzuri ya kufanya uamuzi.
“Mgombea
mwenyewe alizungumza vitu atakavyovifanya ndani ya muda wake wa
uongozi,” alisema.Profesa huyo alifafanua kuwa kwa watu waliopitia
mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), matusi kwao siyo hoja kwani
walishayazoea na kueleza kuwa anayaona kuwa ni masuala mdogo madogo
ambayo hayapaswi kuzingatiwa na kuacha hoja kuu.
Askofu
Mkuu wa Kanisa la Kilutheri Afrika Mashariki (KKAM), Jesse Angowi
alieleza kusikitishwa na maneno hayo ya jazba ambayo hayakustahili
kutamkwa na Mkapa.“Ukawa inao wafuasi wengi tu kama ilivyo CCM.
Mheshimiwa Mkapa amesema kwa jazba na kwa kweli kama kanisa
ametusikitisha kutoa maneno ya kashfa,” alisema.Wakili Peter Shayo
alisema kauli ya Mkapa ni uvunjaji wa wazi wa kanuni za kampeni
zinazowataka wagombea na mawakala wao kutumia lugha ya kistaarabu.
0 comments :
Post a Comment