@nkupamah blog
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Othman
Chande akiongoza maandamano ya Majaji na Watendaji wa Mahakama wakati wa
hafla ya 53 ya kuwapokea na kuwaapisha Mawakili wapya 104 iliyofanyika
katika viwanja vya Karimjee leo jijini Dar es salaam.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Othman
Chande (katikati) akiongoza akiwa na Majaji na Watendaji wa Mahakama
wakiendelea na zoezi zoezi la kuwaapisha Mawakili wapya 104 katika
viwanja vya
Karimjee leo jijini Dar es salaam.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Othman
Chande akizungumza na Mawakili 104 walioapishwa leo jijini Dar es
salaam. Mhe. Chande amewataka Mawakili hao kufanya kazi zao kwa
kuzingatia weledi na maadili ya taaluma yao.
Mawakili wakiwa wamesimama mbele ya Jaji Mkuu kabla ya kuapishwa.
Mawakili walioapishwa wakiwa katika picha ya pamoja na Jaji Mkuu Mhe. Othman Chande na Watendaji wa Mahakama ya Tanzania.
Picha/Aron Msigwa –MAELEZO.
……………………………………………………………………………
Na. Aron Msigwa –MAELEZO
15/12/2015.Dar es salaam.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Othman
Chande amewataka Mawakili kote nchini kufanya kazi zao kwa kuzingatia
weledi na maadili ya taaluma ya Sheria na kwamba wasisite kuwaeleza
ukweli wateja wao wanaopeleka mashauri Mahakamani ili kuepuka kupoteza
muda na gharama katika masuala yanayoweza kupatiwa ufumbuzi nje ya
Mahakama.
Akizungumza na Mawakili wapya 104
waliohitimu Shule ya Sheria kwa mwaka 2015 wakati wa hafla ya 53 ya
kuwapokea na kuwaapisha iliyofanyika katika viwanja vya Karimjee leo
jijini Dar es salaam amesema kuwa msingi mkubwa wa kazi yao umejengwa
katika uzingatiaji wa maadili ya taaluma ya sheria.
Amewataka Mawakili hao kubadilika
kifikra kwa kuwa Mawakili Bora ili kujenga imani na uaminifu kwa jamii
wanayoihudumia na kuongeza kuwa
sasa wameingia kwenye utaratibu wa
kutambuliwa rasmi na Mahakama ya Tanzania kwa kuwezeshwa kufanya
shughuli za uwakili kwenye mahakama ya Tanzania maeneo mbalimbali
nchini.
“Naomba mtambue kuwa kila Wakili
ni Ofisa wa Mahakama hivyo mnao wajibu na jukumu la kusoma, kufuatilia
mashauri mbalimbali ili kuwa na uhakika wa kesi mnazosimamia kuliko
kuzitegemea Mahakama”
Aidha, ameeleza kuwa yapo mambo
ambayo yamekua yakifanywa na baadhi ya Mawakili wasio waaminifu
yanayochafua sura ya Taaluma ya Sheria ikiwemo kutumia nyaraka za
kughushi, kuvunja Kanuni na Maadili ya Taaluma huku baadhi yao
wakijikuta wakiingia katika mgogoro na Mamlaka zinazosimamia kitaaluma
taaluma hiyo.
“Nawataka mzingatie sheria, kanuni
na Maadili ya Uwakili, hata hivyo tuna chombo kinachosimamia maadili
yenu, wapo takribani 176 waliokiuka maadili na hawa wanashughulikiwa kwa
mujibu wa Sheria ili kulinda maadili na utendaji wa taluma yenu”
Amesisitiza Mhe. Othman.
Amewataka watimize wajibu wao
kwanza kwa wananchi watakaouhudumia pamoja na Mahakama ya Tanzania
ambayo inawataka kufanya kazi zao kwa kuzingatia Sheria, kanuni na
taratibu zilizowekwa.
Mhe. Othman amefafanua kuwa
Mahakama ya Tanzania inaendelea na Mkakati wa kupunguza mrundikano wa
Kesi Mahakamani kwa kuhakikisha kuwa kesi zote zinazofikishwa
Mahakamani zinamalizika katika kipindi cha chini ya mwaka 1
Ameeleza kuwa silimia 47 ya kesi
zaidi ya 200 zilizokuwepo Mahakama Kuu katika kipindi cha miaka 4
iliyopita zimeendelea kusisikilizwa kwa ubora na sasa zimebaki asilimia
17 ya kesi hizo jambo linaonyesha kuongezeka kwa ufanisi wa Mahakama.
Kwa upande wake Mwanasheria Mkuu
wa Serikali Mhe. George Masaju akiwakaribisha Mawakili hao katika
familia ya sheria Tanzania amesema kuwa katika jamii wanao mchango
mkubwa katika kuhakikisha Haki na Usawa vinadumishwa nchini.
Amesema mawakili hao kabla ya
kuapishwa na kuingizwa kwenye utaratibu wa kutambuliwa kuwa Mawakili
wamepitia na kufauru vigezo vya kitaaluma vilivyowekwa ili kulinda
heshima ya Taaluma ya sheria nchini.
Amewaeleza kuwa mara baada ya
kupokea viapo vyao wameingia kwenye utumishi wa umma kutekeleza majukumu
yao ya kikatiba na kuongeza kwamba wao kama wanasheria wanatakiwa
kuzingatia weledi wa taaluma yao.
Amewataka kuwa makini katika
utendaji wao kwa kuepuka kuwa sehemu ya migogoro na kuepuka kuegemea
upande wowote watakapokuwa wakitimiza majukumu yao ili kuendelea kujenga
jamii ya kistaarabu na ya kidemokrasia.
” Naomba mkumbuke kuwa mna wajibu
mkubwa kwa watu mtakaokuwa mnawahudumia, zingatieni maadili maana ninyi
sasa ni sehemu ya Mahakama ya Tanzania, fanyeni kazi kwa weledi na
umakini mkubwa” Amesisitiza.
Amesema utekelezaji wa majuku yao
ya kila siku ni sehemu ya utumishi wao katika umma hivyo wasiruhusu aina
yoyote ya ukiukwaji wa maadili yakitika kutimiza majukumu yao na
kuwasaidia wananchi wasiokuwa na kipato/ wananchi masikini watakakao
omba msaada wao wa kisheria.
Aidha amewataka wawe wabunifu,
kufanya kazi kwa bidii na kujiendeleza pale inapowezekana ili waweze
kuwa msaada kwa wananchi walio na kiu ya kupata huduma kutoka kwao.
Kwa upande wake Rais wa Chama cha
Wanasheria Tanganyika (TLS) Charles Rwechungura akizungumza wakati wa wa
kuwakaribisha mawakili hao 134 amesema kuwa wao kama Chama cha
Wanasheria wanayofuraha ya kuwakaribisha wanachama wapya kwenye uwanja
wa Sheria nchini.
Amesema mawakili hao wameingia
katika wakati muafaka kuongeza nguvu katika kuwahudumia wananchi huku
akieleza kuwa shule ya Wanasheria Tanzania itaendelea kutoa mafunzo na
kusimamia viwango vya taaluma ya sheria nchini na kuwataka mawakili hao
kulinda heshima ya taaluma ya sheria kwa kutoa huduma bora kwa umma.


0 comments :
Post a Comment