Nkupamah media:
Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza na viongozi serikali na kisiasa jijini Tanga jana,
Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, alisema serikali italazimika
kuivunja halmashauri hiyo endapo mgogoro huo hautamalizwa haraka,
kutokana na ukweli kwamba tangu kuanza kwa uongozi wa awamu ya tano
baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana imeshindwa kufanya vikao vyake
halali kwa mujibu wa katiba kutokana na mgogoro wa kisisa baina ya Chama
Chama cha Mapinduzi (CCM) na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa, huku
wananchi wakishindwa kutatuliwa kero zao kwa wakati hivyo kuzorotesha
maendeleo yao.
“Mpaka sasa jiji la Tanga hakuna uongozi uliosimama, sasa hatuwezi
kwenda kwa mwendo huu, wananchi wanahitaji maendeleo na kurudia uchaguzi
hatuwezi ni gharama kubwa, kilichobaki ni kuivunja halmashauri mpaka
hapo muda wa kufanya uchaguzi kwa mujibu wa katiba ya nchi utakapotimia,
hivyo kwa maana nyingine kama itavunjwa serikali kuu ndiyo itasimamia
shughuli za jiji hili,” alisema Suluhu.
Alisema mkoa huo una mipango mbalimbali ya maendeleo lakini haiwezi
kutekelezeka kutokana na mgogoro uliopo na kuwataka viongozi wa mkoa
kwa kushirikiana na wazee kukaa chini kutafuta namna ya kuumaliza
haraka.
“Jiji ni kioo cha mkoa mzima, sasa kama wazee hawatakaa kitako na
viongozi kutafuta suluhu, basi hii mipango yenu yote ya kufufua viwanda
itakuwa ni ndoto tu kwa sababu hapa mjini hakupo shwari na tunalitambua
hilo,” alisema.
Mgogoro wa umeya Tanga umeibuka baada ya CCM yenye madiwani
wachache kushinda nafasi hiyo dhidi ya Ukawa yenye madiwani wengi jambo
ambalo linapingwa na umoja huo unaondwa na vyama vya CUF, Chadema,
NCCR-Mageuzi na NLD.
Hatua kama hiyo ya kuvunja halmashauri si mara ya kwanza kutokea
nchini, kwani mwaka 1996, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam
ilivunjwa na serikali na badala yake ikaundwa Tume ya Jiji iliyokuwa
chini ya Charles Keenja.
MAGENDO
Makamu wa Rais pia aliema mkoa wa Tanga unakabiliwa na changamoto
kubwa ya biashara ya magendo, hali ambayo inarudisha nyuma mkoa huo
kiuchumi na kimaendeleo.
Kufuatia hatua hiyo aliiagiza kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa
huo kutumia kila mbinu kuzuia biashara hiyo ili mkoa uweze kuimarika
kiuchumi na kimapato.
AONYA UHABA WA CHAKULA
Kuhusiana na suala la chakula, Makamu wa Rais alisema serikali ya
awamu ya tano haitamvumilia mkuu wa mmoa yeyote wala wilaya ambaye
atatoa malalamiko ya kukosekana kwa chakula kwenye eneo lake na badala
yake atakuwa amejifukuzisha kazi mwenyewe.
Alisema kukosekana kwa chakula wakati viongozi wa eneo husika wana
uwezo wa kujenga malambo ili kukinga maji ya mvua kipindi cha masika na
kuwaelekeza wananchi kulima mazao yanayostahimili ukame, itakuwa ni
kipimo chao cha uongozi na wale ambao watashindwa kupata madawati kwa
ajili ya shule kwenye maeneo yao.
Awali akisoma taarifa ya mkoa wa Tanga kwa Makamu wa Rais, Mkuu wa
Mkoa wa Tanga, Mwantumu Mahiza, alisema hali ya chakula mkoani humo hadi
kufikia mwezi huu si ya kuridhisha kutokana na kuchelewa kunyesha kwa
mvua msimu wa mwaka 2014/2015 na hata ziliponyesha hazikuwa na
mtawanyiko mzuri.
0 comments :
Post a Comment