Nkupamah media:
Siku
nne baada ya majambazi 12 kuvamia Benki ya Access tawi la Mbagala,
jijini Dar es Salaam na kuiba Sh. milioni 20 na kusababisha vifo vya
watu sita, mtu anayedaiwa kuwa kinara wa uhalifu huo ametiwa mbaroni
baada ya kutajwa na washirika wake, akiwamo aliyekamatwa akiwa anafunga
ndoa.
Taarifa za uhakika ambazo gazeti hili ilizipata zinaeleza kuwa,
kinara wa ujambazi huo alikamatiwa Sinza Mori, wilaya ya Kinondoni jana,
saa 11:00 jioni.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo Nipashe ilizipata, kikosi
kinachoshirikisha askari wa majeshi mbalimbali ikiwamo, polisi na la
wananchi wa Tanzania, kilinasa watu wanne kwenye sherehe ya harusi baada
ya kufuatilia mawasiliano yao ya simu.
“Unajua sasa hivi hili suala linahusisha jeshi ambao wamefuatilia
kwenye mtandao na kunasa simu za watu wanne ambao wamekamatwa huko
Mbagala, akiwamo bwana harusi na watu wengine wanne,” kilisema chanzo
chetu.
Taarifa hizo zinasema baada ya watu hao kukamatiwa wakiwa wanafunga
ndoa msikitini, walisaidia kutoa taarifa ambazo hatimaye zilifanikisha
kukamatwa kwa mtu huyo anayedaiwa kuwa ni kinara wa ujambazi huo.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro,
alipoulizwa kuhusu tarifa hizo alisema bado hajazipata na kwamba
yawezekana wasaidizi wake wamemkamata lakini bado hawajamfikishia
taarifa.
“Sina chochote hadi sasa ningekuwa nacho kwa nini nikunyime wakati ni jambo la sifa kwetu,” alisema Kamanda Sirro.
Kinara huyo amekamatwa ikiwa imepita siku moja baada ya Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, kutangaza uwezekano wa kutumia
Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kushirikiana na polisi kuwasaka
wahalifu wote waliojificha kwenye misitu ya Bagamoyo na Pwani, ambako
inadaiwa walikimbilia baada ya tukio la Mbagala.
Pia waziri huyo alisema katika operesheni hiyo, watakuwa
wakiwasimamisha mara kwa mara watumia pikipiki kwa sababu vyombo hivyo
vimekuwa vikitumiwa na majambazi katika kufanikisha matukio yao.
TUKIO LILIVYOKUWA
Juzi Kamanda Sirro alisema majambazi hao wakiwa na silaha aina ya
SMG na mabomu matatu ya kutupa kwa mkono yaliyotengenezewa Russia,
walifika kwenye benki ya Access tawi la Mbagala wakiwa na pikipiki sita.
Alisema kila pikipiki ilikuwa na majambazi wawili na baada ya
kuwasili eneo hilo walishambulia polisi waliokuwa nje wakilinda benki
hiyo.
“Walivamia chumba cha askari nje ya benki na kumuua kwa kumpiga
risasi kichwani askari wetu na kumjeruhi mwingine eneo la maungoni,
kisha kuchukua silaha na kuingia ndani ya benki,” alisema.
Alisema baada ya kuingia ndani, walimshambulia mlinzi binafsi wa
kampuni ya ulinzi ya Security Group of Afrika, Baraka Fredrick maarufu
kama Selemia, ambaye alifariki papo hapo.
Pia alisema majambazi hao waliwashambulia na kuwajeruhi kwa risasi
wafanyakazi wawili wa benki hiyo ambao ni Ofisa Mikopo, Salum Juma na
Francis Amani waliokuwa chumba cha kuhifadhia fedha (Strong Room).
“Walipiga ‘Safe’ yakuhifadhia fedha lakini haikufunguka ndipo
wakaamua kwenda kaunta na kufanikiwa kupata Sh. milioni 20 na kuondoka
nazo,” alisema.
Alisema wakati wanaondoka walifyatua risasi iliyompata kidevuni
Abdi Salum maarufu kama Shemdoe ambaye ni muuza duka jirani na benki
hiyo.
Kamanda Sirro alisema jeshi la polisi lilikuwa limejiimarisha
kiulinzi maeneo hayo, vikiwamo vikosi vya farasi , pikipiki na magari,
walianza kuwafuatilia majambazi hao ambao wakati huo walikuwa wakitumia
usafiri wa pikipiki.
Alisema katika majibizano ya risasi polisi waliwaua majambazi watatu na kufanikiwa kupata SMG tatu na pikipiki sita.
Alisema majambazi wengine walikimbia kwa miguu na kuziacha pikipiki hizo, lakini fedha zilizoibwa hawakufanikiwa kuzipata.
Kamanda Sirro alisema vikosi vyake viliendelea kuwafukuza majambazi wengine hadi msitu wa Kongowe unaotokea mkoa wa Pwani.
“Majambazi hao walitokomea ndani ya msitu huo na polisi tunaendelea kuwasaka na tunaahidi kuwakamata,” alisema.
Aliongeza kuwa, walishindwa kuwapiga risasi wakati wakiwakimbiza kwa kuhofia kujeruhi wananchi wengi waliokuwa eneo hilo.
“Ili kuonyesha majambazi hawa walikuwa wamejipanga, walitumia mbinu
ya kivita kwa kuvamia wakiwa na mabomu ili waliovamiwa wasipate msaada,
askari wetu aliyejeruhiwa ambaye amelazwa Muhimbili alifanya kazi kubwa
licha ya majeraha aliyopata,” alisema.
0 comments :
Post a Comment