Nkupamah media:
Mwenyekiti
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe,
amemshitaki Rais John Magufuli mbele ya maaskofu kadhaa wa Kanisa la
Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).
Mbowe amedai kuwa Serikali yake ya Awamu ya Tano imekuwa ikiwatimua
watumishi mbalimbali wa umma bila kuwapa nafasi ya kuwasikiliza kupitia
kampeni ya kupambana na ufisadi, inayotambulishwa kwa kaulimbiu ya
‘utumbuaji majipu’.
Akizungumza jana katika ibada maalumu ya shukrani kwa kumaliza
uchaguzi mkuu salama, iliyofanyika kwenye Usharika wa Nshara wa Dayosisi
ya Kaskazini ya KKKT na kuhudhuriwa na Mkuu wa KKKT, Askofu Dk.
Frederick Shoo, na maaskofu wastaafu Dk. Erasto Kweka na Dk. Martin
Shao, Mbowe alisema (wapinzani) hawaridhishwi na hatua ya serikali ya
Rais Magufuli kuendeleza timuatimua na kuwasimamisha kazi watumishi wa
umma 160 tangu aingie madarakani bila kuwapa nafasi ya kuwasikiliza.
Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni,
alisema wapinzani wako tayari kuipongeza serikali wakati wowote
inapofanya mambo mazuri kwa manufaa ya taifa, lakini kwa sharti kwamba
mara zote iwe inahakikisha sheria za nchi zinasimamiwa, mali na
rasilimali za umma zinalindwa na kila kitu kinafanyika kwa kuzingatia
taratibu zilizopo.
"Kutokana na hali ya sintofahamu kutamalaki katika taifa kwa sasa,
hakuna mtumishi wa umma aliye na amani kutokana na mfumo unaoitwa
kutumbua majipu. Tunasikia watumishi wa umma wakifukuzwa kazi bila
kusikilizwa.
“Mpaka sasa kuna watumishi 160 wamefukuzwa na wengine kusimmishwa.
Lakini pia zaidi ya taasisi na idara za serikali zipatazo 20 hazina
uongozi…hii si sahihi,” alisema.
Katika ibada hiyo, Mbowe alikuwa ameongozana na wabunge 16 na
makada wengine mbalimbali wa Chadema, alitoa sadaka ya Sh. milioni 279
kwa ajili ya kusaidia ukarabati na upanuzi wa jengo la Bethel lililoko
Hai.
"Sisi tunamshukuru Mungu leo kwa kuwa tuko salama ndiyo maana
tunatoa sadaka. Sadaka yetu tunaielekeza kwenye upanuzi na ukarabati wa
jengo hili la Betheli la Usharika wa Nshara. Kwa hiyo, nawaomba sana
viongozi wa dini na Watanzania kuliombea taifa kutokana na hali
inayoendelea," alisema Mbowe.
Kiongozi huyo ambaye pia ni Mbunge wa Hai, alisema wabunge 42 wa
Chadema wamemuunga mkono kwa kuchangia kanisa hilo Sh. milioni 131.5;
mwanasiasa mkongwe na mfanyabiashara, Philemon Ndesamburo alimchangia
Sh. milioni 50; marafiki zake wa Arusha Sh. milioni 49.9; Mwenyekiti
mstaafu wa Chadema, Edwin Mtei Sh. milioni mbili; makada wengine wa
Chadema Sh. milioni 15 na Kamati ya Maandalizi Sh. milioni 41.
Katika hatua nyingine, Mbowe alitumia nafasi hiyo pia kuzungumzia
mgogoro wa uchaguzi wa kumpata Meya wa Jiji la Dar es Salaam kwa
kuitupia lawama CCM kwa madai kuwa ndio wanaokwamisha kwa maslahi yao.
Alisema jambo hilo pia linasikitisha kwa sababu sasa ni miezi minne
imepita huku haki ya wananchi wa Jiji la Dar es Salaam kuwa na Meya wao
ikiendelea kuminywa kutokana na CCM kutoheshimu demokrasia na kutaka
waendelee kuongoza licha ya wananchi kufanya uamuzi wao kupitia sanduku
la kura katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana.
Chadema na Chama cha Wananchi (CUF) vinavyoshirikiana kupitia Umoja
wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ndivyo vyenye idadi kubwa ya madiwani
kulinganisha na CCM, hivyo kwa mujibu wa Mbowe, CCM wamebaini kuwa
hawawezi kushinda na sasa wanajitahidi kadri wawezavyo kukwamisha
uchaguzi huo.
ASKOFU SHOO AZUNGUMZIA UTUNZAJI MAZINGIRA
Awali, akihubiri katika ibada hiyo, Askofu Dk. Shoo alielezea kusikitishwa kwake na uharibifu wa mazingira unaoendelea nchini.
Alisema takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 60 ya eneo la ardhi liko
katika hatari ya kugeuka jangwa na dalili zake ni kuongezeka kwa joto
duniani na mabadiliko ya tabia nchi.
"Bado hatujawa mawakili wema wa mazingira. Ukame, mafuriko, kupotea
kwa rutuba na ubora wa ardhi na mabadiliko ya tabia nchi ni matokeo ya
sheria za mazingira kutosimamiwa ipasavyo kukabiliana na hali hii.
Sheria ziko nyingi, lakini hakuna utayari wa moja kwa moja wa kuwajibika
katika kuzitekeleza," alisema Askofu Shoo.
Akifafanua Zaidi, kuhusu uharibifu huo, Dk. Shoo alisema zaidi ya
hekta 400,000 za misitu huteketea kila mwaka, ndiyo maana kanisa
limeamua kujikita katika kutoa elimu na kupiga kelele ili mamlaka
zinazohusika zichukue hatua.
0 comments :
Post a Comment