CHAMA
Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimefurahishwa na kimepata matumaini
makubwa kutokana na taarifa ya Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China
ambayo imeelezea dhamira yake ya kuendelea kushirikiana na Tanzania na
Zanzibar katika jitihada zake za kuimarisha uchumi na ustawi wa jamii.
Kauli
hiyo ya Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kwa mara nyengine tena
inathibitisha imani ya kweli ya nchi hiyo katika kuendeleza ushirikiano
wa kindugu baina ya nchi zetu mbili ambao umedumu kwa zaidi ya nusu
karne sasa.
CCM
inayo kila sababu ya kuthamini uhusiano wetu na ndugu zetu wa China
siyo tu kwa sababu ya misaada ya nchi hiyo ya kiuchumi na kijamii ambayo
imekuwa ikitoa msukumo mkubwa katika maendeleo ya Zanzibar na Tanzania
kwa jumla, lakini pia kutokana na dhamiri ya kweli ya nchi hiyo katika
kusaidia maendeleo ya wananchi wetu na taifa wakati wa dhiki na vile
vile wakati wa faraja. Huu ndio urafiki wa kweli.
Zanzibar
bado inakumbuka ya msaada mkubwa wa nchi hiyo, iliyowahi kutolewa
katika kujenga na kuviendeleza viwanda mbali mbali ikiwemo kiwanda cha
sukari na manukato cha Mahonda, kiwanda cha ngozi na viatu kilichokuwepo
Maruhubi, usambazaji wa mabomba ya maji safi na salama katika maeneo
mbali mbali Unguja na Pemba, uimarishaji wa kilimo Upenja, Bambi na
maeneo mengine mengi
Jamhuri
ya Watu wa China kwa karibu miaka 50 sasa imekuwa ikituma madaktari
wake kuja Zanzibar kusaidia huduma za matibabu kwa wagonjwa
wanaosumbuliwa na maradhi mbali mbali katika hospitali kuu ya Mnazi
Mmoja na Abdalla Mzee iliyoko Pemba. Huduma za madaktari hao kwa
kushirikiana na madaktari wazalendo zimekuwa zikisaidia kuimarisha afya
na kuokoa maisha ya wananchi kadhaa hapa nchini.
Mradi
wa ujenzi wa hospitali kubwa ya kisasa ya Abdalla Mzee huko Mkoa wa
Kusini Pemba unaofadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China pia
unathibitisha dhamira ya nchi hiyo katika kuunga mkono jitihada za
Serikali katika kuimarisha sekta ya jamii. Ni dhahiri mradi huu baada ya
kukamilika utaleta sura mpya kwa Pemba.
Ujenzi
wa Uwanja wa Kisasa wa Michezo wa Amani pamoja na marekebisho yake
yaliyofanywa katika miaka ya hivi karibuni pamoja na maandalizi ya
Ujenzi wa kiwanja cha mpira wa miguu cha Mao Tse-tung, kiliopo Mjini
Zanzibar ni miongoni mwa misaada ya China.
Vituo
vya kurushia matangazo ya Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC) vya
Radio iliyopo maeneo ya Rahaleo na Dole vimejenga kwa msaada wa Serikali
ya Jamhuri ya Watu wa China.
Zanzibar
na Tanzania kwa ujumla, kwa muda wote zimekuwa zikifaidika kwa kupatiwa
nafasi za masomo kwa vijana wake ya taaluma tofauti nchini China ya
muda mfupi na mrefu.
Kutokana
na dhamira yake hiyo, Chama cha Mapinduzi siku zote kimekuwa
kikijivunia ushirikiano wake na Chama cha Kikomunisti cha China (CCP) na
kitaendelea kufanya hivyo daima kwa maslahi ya pande zote mbili, kwa
kufahamu kwamba itikadi na msimamo thabiti wa CCP mbele ya mataifa
mengine duniani, ndio uliyoifanya China leo kuwa moja kati ya mataifa
yenye nguvu kubwa kiuchumi duniani.
Uhusiano
wetu na China ambao uliasisiwa mara baada ya uhuru wa Tanganyika kwa
Tanzania Bara na Mapinduzi ya tarehe 12 Januari 1964 kwa Zanzibar,
umejengwa kwa misingi ya haki, usawa, kuheshimiana pamoja na kuzingatia
na kujali maslahi ya kila upande.
Aidha,
Chama Cha Mapinduzi kinatoa pongezi za dhati kwa nchi mbali mbali
duniani zinaoungana na Zanzibar na Tanzania kwa kuendelea kuimarisha
umoja na uhusiano mwema kwa maslahi ya wananchi walio wengi wa pande
zote mbili za nchi hizo.
………………
VUAI ALI VUAI
NAIBU KATIBU MKUU WA CCM ZANZIBAR
APRILI 4, 2016
0 comments :
Post a Comment