Waziri wa
Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry amefanya ziara ya kihistoria
kwenye makumbusho ya wahanga wa bomu la atomiki lililorushwa kwenye mji
wa Japan, Hiroshima, wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.
Kerry
ambaye aliongozana na mawaziri wenzake wa mambo ya nchi za nje wa kundi
la mataifa saba tajiri duniani-G7, za Uingereza, Ufaransa, Canada,
Ujerumani, Italia na Japan kuzuru makumbusho hayo, anakuwa
mwanadiplomasia mwandamizi wa kwanza wa Marekani kuzuru eneo hilo na
ameelezea jinsi alivyoguswa katika ziara hiyo ya Hiroshima.
''Nataka
kuelezea binafsi jinsi nilivyoguswa sana na heshima niliyopata kuwa
waziri wa kwanza wa mambo ya nje wa Marekani kuzuru mji huu mzuri wa
Hiroshima. Mapema leo kama mnavyojua, niliungana na Waziri wa Mambo ya
Nje wa Japan, Fumio Kishida pamoja na mawaziri wengine katika ziara yetu
kwenye makumbusho haya ya ajabu ya amani,'' alisema Kerry.
Akizungumza
na waandishi wa habari baada ya kuweka shada la maua kwenye makumbusho
hayo, Kerry amesema kila mmoja anatakiwa kuzuru mji wa Hiroshima, ambako
zaidi ya Wajapan 140,000 waliuawa kwa bomu la atomiki ambalo
lilidondoshwa na Marekani Agosti 6, 1945.
Ziara
hiyo inaonekana kama inaongeza matarajio huenda Rais wa Marekani, Barack
Obama akazuru eneo hilo mwezi ujao, wakati atakapohudhuria mkutano wa
kilele wa mwaka wa viongozi wa mataifa yanayounda kundi la G7, nchini
Japan.
Ziara imefanyika pembezoni mwa mkutano wa mawaziri wa G7
Ziara
hiyo imefanyika baada ya mawaziri hao wa mambo ya nje wa kundi la G7
kumaliza mkutano wao wa siku mbili ambapo kwa pamoja wamekubaliana
kushinikiza kuwepo na dunia isiyotumia silaha za nyuklia. Wanadiplomasia
hao waandamizi wa kundi la G7 wamesema katika azimio lao la pamoja
kwamba wanathibitisha dhamira yao ya kuwepo na dunia salama kwa wote na
kwa kujenga mazingira ya dunia isiyokuwa na silaha za nyuklia, ambazo
kwa njia moja ama nyingine husababisha kukosekana kwa utulivu wa
kimataifa.
Kerry
amesema ana matumaini ziara hiyo inaonyesha umuhimu wa kukuza amani na
kuimarisha uhusiano wa washirika imara ambao wameujenga pamoja kwa ajili
ya kuwa na dunia iliyo salama na kushirikiana kuhakikisha dunia haina
silaha za maangamizi.
Kauli
hiyo inaonyesha makubaliano yaliyofikiwa kwenye mazungumzo ya mawaziri
hao na kuhusu majaribio ya ufyatuaji wa makombora yaliyofanywa hivi
karibuni na Korea Kaskazini, ambapo wamesema hivyo ni vitendo vya
kiuchokozi. Siku ya Jumamosi, Korea Kaskazini ilisema imefanikiwa
kufanya jaribio la kombora lake ambalo linaweza kuishambulia Marekani.
Kerry
amesema leo kuwa Marekani imejiandaa kuongeza shinikizo kwa Korea
Kaskazini baada ya vitendo vyake vya uchokozi vya hivi karibuni, lakini
bado imeacha milango wazi kwa ajili ya mazungumzo. Amesema bado kuna
uwezekano wa kuongeza shinikizo zaidi, kulingana na vitendo vya Korea
Kaskazini, lakini wameweka wazi kwamba wamejiandaa kwa mazungumzo ya
amani. (P.T
0 comments :
Post a Comment