Picha: Kikao cha Bunge la Burundi
------------------
BURUNDI
Wabunge wa Burundi wamepinga azimio nambari 2303 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kukataa kabisa suala la kutumwa nchini humo askari polisi 228 wa kimataifa.
------------------
BURUNDI
Wabunge wa Burundi wamepinga azimio nambari 2303 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kukataa kabisa suala la kutumwa nchini humo askari polisi 228 wa kimataifa.
Katika kikao chake cha jana, Bunge la Burundi lilipinga azimio hilo la Baraza la Usalama na kutangaza kuwa uamuzi huo wa Umoja wa Mataifa hauendani na mtazamo wa serikali ya Bujumbura.
Wabunge wameeleza kuwa uamuzi wa kutaka kutuma kikosi cha askari polisi nchini Burundi umechukuliwa bila ya kushauriana na serikali ya nchi hiyo.
Taarifa ya Bunge la Burundi inasema, katika mpango huo haikuzingatiwa na kutiliwa maanani hali ya kisiasa na kiusalama ya nchi hiyo.
Kwa mujibu wa azimio hilo ambalo lilipendekezwa na Ufaransa, askari polisi 228 wa Umoja wa Mataifa watatumwa nchini Burundi kwa shabaha ya kurejesha amani na kulinda haki za binadamu nchini humo kwa kipindi cha mwaka mmoja. Muda wa huduma za kikosi hicho utaongezwa iwapo hali itakuwa mbaya zaidi.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pia limeihimiza serikali ya Burundi kufanya mazungumzo na makundi yote ya upinzani wakiwemo wapinzani walioko nje ya nchi kwa lengo la kukomesha mgogoro wa ndani ya nchi hiyo.
Azimio hilo la Baraza la Usalama limekabiliwa na upinzani mkubwa wa wananchi huko Burundi na ripoti zinasema kuwa, maandamano dhidi ya Ufaransa ambayo ndiyo iliyopendekeza muswada wa azimio hilo, bado yanaendelea.
Msemaji wa serikali ya Burundi, Philippe Nzobonariba ametangaza kuwa, suala la kutumwa askari polisi wa Umoja wa Mataifa nchini humo ni kinyume na sheria za kimataifa zinazolinda mamlaka ya kujitawala nchi wanachama.
Kabla ya hapo Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi alikuwa amesema kwamba, kutumwa askari wa kimataifa nchini humo ni kuingilia masuala ya ndani ya Burundi na kwamba nchi yake itakabiliana nao kama wavamizi.
Mgogoro wa ndani nchini Burundi unaendelea kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa na juhudi za kikanda na kimataifa za kujaribu kukomesha machafuko na ghasia nchini humo bado hazijazaa matunda. Machafuko hayo yalishika kasi baada ya kiongozi wa sasa wa nchi hiyo kutangaza kuwa atagombea kiti cha rais kwa mara ya tatu hapo mwaka jana. Suala hilo lilipingwa na vyama vya kisiasa vya upinzani vikisema ni ukiukaji wa katiba na makubaliano ya amani ya Arusha.
Hali hiyo imezidisha machafuko ya ndani kwa kadiri kwamba, Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, serikali ya Bujumbura imezidisha mateso na unyanyasaji dhidi ya wakosoaji na wapinzani wake. Vilevile ripoti zinasema kuwa askari wa Burundi wanahusika na visa vingi vya kuwabaka na kuwanajisi wanawake wanaoshikiliwa na vyombo vya usalama.
0 comments :
Post a Comment