BARAZA la Mitihani la Tanzania (NECTA)
limesitisha mpango wa kuwafanyia mtihani wa udahili wanafunzi wote
waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu katika shule za
sekondari za serikali uliokuwa ufanyike Februari 28, mwaka huu.
Naibu Katibu Mtendaji wa Necta, Athumani
Salumu alisema hayo juzi kwenye kikao cha wadau wa sekta ya elimu Mkoa
wa Morogoro alipokuwa akihitimisha mada yake kwa wajumbe wa kikao hicho
kilichoongozwa na mkuu wa mkoa huo, Dk Stephen Kebwe.
Salumu alisema mpango wa kuwafanyia
mtihani wa udahili wanafunzi hao ulitokana na matakwa yaliyowasilishwa
Necta na baadhi ya wakuu wa shule za serikali wakipendekeza kupitia
maofisa elimu wa mikoa na wilaya kuwa wanafunzi wa kidato cha kwanza
waliochaguliwa na kupangiwa shule zao wengi hawana sifa na uwezo wa
kumudu masomo.
Naibu Katibu Mtendaji wa Necta alisema
wakuu wa shule walikuwa wakiomba kupata idhini ya kuwafanyia mtihani
wanafunzi ili kubaini uwezo wao na kwamba baraza liliwasiliana na
maofisa elimu mkoa na wilaya likiwataka kuwasilisha orodha ya idadi ya
wanafunzi wa kidato cha kwanza waliopangiwa kwenye shule ya zao.
Alisema baada ya kufahamika idadi ya
wanafunzi hao, baraza ndilo litatunga maswali ya mitihani yenye
kuzingatia mfumo na vigezo maalumu na kutumiwa wakuu wa shule hizo ili
kuusimamia kwa lengo la kuweka uzani sawa wa mtihani huo.
Alisema moja ya masharti ni kwamba
mtihani huo ulitakiwa ufanyike kwa wanafunzi wa kidato hicho kwa shule
zote za serikali siku moja na kwa muda uliopangwa.
Hata hivyo, alisema baada ya kuwatumia
masharti hayo, wakuu wa shule hizo walishindwa kuwasilisha orodha ya
wanafunzi kwa maofisa elimu wa mikoa na wilaya ili itumwe Necta na
kutokana na mazingira hayo, baraza limeamua kusitisha kuwadahili
wanafunzi wa kidato cha kwanza na kuitaka mamlaka inayosimamia elimu
kuendelea na utaratibu wao wa kawaida.
“Necta imewasiliana na wahusika kwa
barua rasmi ya kusitisha mtihani huo ambao ulipangwa ufanyike Februari
28, mwaka huu na wanafunzi wote waliopangiwa kidato cha kwanza shule
mbalimbali za serikali zikiwemo za bweni, waendelee na masomo kama
yalivyopangwa,” alieleza Naibu Katibu Mtendaji wa Necta.
Novemba mwaka jana, serikali ilitangaza
kuwa wanafunzi 526,653 sawa na asilimia 94.8 ya waliofaulu mtihani wa
darasa la saba mwaka jana, wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza
katika shule za sekondari za serikali katika awamu ya kwanza huku 28,638
wakishindwa kupangiwa shule katika awamu ya kwanza.
Kati ya wanafunzi hao, wasichana ni
268,052 sawa na asilimia 94.5 ya wasichana waliofaulu na wavulana ni
258,601 sawa na asilimia 95.2 ya wavulana waliofaulu.
0 comments :
Post a Comment