Mfanyabiashara maarufu Yusuf Manji amewasilisha hati ya kuiomba Mahakama Kuu iwaagize maofisa Uhamiaji wamfikishe mahakamani ili kesi yake isikilizwe kwa mujibu wa sheria.
Manji yuko kwenye matibabu Hospitali ya Aga Khan jiji hapa akiwa chini ya ulinzi baada ya kuachiwa kwa dhamana.
Februari 20 mwaka huu, alipelekwa ofisi ya Uhamiaji mkoa na kuhojiwa kwa madai ya kuingia nchini kinyume cha sheria.
Katika kesi hiyo wajibu maombi hayo ni Kamishna Mkuu wa Uhamiaji, Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam,Mwanasheria Mkuu wa Serikali(AG) na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam.
Wakili wa Manji, Hudson Ndusyepo aliyefungua kesi ya maombi hayo, anataka Mahakama iagize maofisa uhamiaji na polisi kumfikisha mahakamani ili iamue uhalali wa kushikiliwa kwake na kuagiza aachiwe.
Katika hati ya maombi hayo, Ndusyepo anadai kuwa alimtembelea mteja wake hospitali ya Aga Khan Februari 17 mwaka huu na kukuta maofisa wa Uhamiaji wakimsubiri mteja wake wampeleke kwa ofisa Uhamiaji wa mkoa kwa mahojiano dhidi ya tuhuma kuwa siyo raia wa Tanzania.
Kwa mujibu wa Ndusyepo, Manji ambaye ni Mwenyekiti wa Quality Group Limited na Diwani wa Mbagala Kuu, Amedai kuwa alitoa maelezo kwa maofisa Uhamiaji na alirudishwa Aga Khan ambako yupo chini ya ulinzi hadi leo.
0 comments :
Post a Comment