JESHI la Polisi jijini Dar es Salaam limetakiwa kumfikisha Mahakamani, Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, badala ya kuendelea kumuweka Mahabusu, anaandika Hamisi Mguta.
Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), alikamatwa jana jijini Dar es Salaam akiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere akituhumiwa kwa makosa ya uchochezi ambapo alikuwa akielekea jijini Kigali, Rwanda kuhudhuria kikao cha halmashauri ya vyama vya wanasheria wa Afrika Mashariki (EALS) kilichoanza leo..
Kauli ya kutaka Lissu afikishwe mahakamani imetolewa leo na Fatma Karume, Mwanasheria wa Tundu Lissu alipozungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada kutoka kituo kikuu cha Polisi, kanda maalum ya Dar es Salaam ambapo Tundu Lissu alikuwa akihojiwa baada ya kukamatwa na kulala mahabusu.
“Tumeamua, tutalipeleka jeshi la polisi Mahakamani kuiomba mahakama iiambie jeshi la polisi imlete mahakamani jumatatu ili kama wana kesi waendelee na kumkabidhi Tundu Lissu kwa mahakama, wamuachie au wamapeleke mahakamani,” amesema.
Wakili Fatma amesema hakuna sababu yoyote ya kumnyima dhamana Lissu na kuwa jeshi la polisi halijasema kama Lissu amefanya uchochezi kwa nani na alichochea afanye jambo gani.
“Nilimuuliza ndani kwamba Tundu Lissu mtampeleka mahakamani lini wakaniambia hawajui na bado wanaendelea kufanya upelelezi, ina maana nchi hii tunakamata kwanza kisha upelelezi baadaye?,” alihoji.
Hata hivyo, taarifa zinaeleza kuwa Polisi wamemchukua Lissu kutoka kitoani hapo kuelekea naye nyumbani kwake kwa ajili ya kupekuliwa ambapo hadi Mtandao huu unapata taarifa hizo haijulikani upekuzi huo ulihusu kitu gani.
0 comments :
Post a Comment