Na Beatrice Lyimo-Maelezo
Dar es Salaam
Asilimia 49 kati ya asilimia
100 ya matokeo ya uchunguzi wa makosa ya vinasaba (DNA)
yanayowasilishwa katika ofisi ya Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa
Serikali kwa mwaka yanaonyesha kuwa baba si mzazi halali wa mtoto katika
kesi hizo.
Hayo yamesemwa na Mkemia Mkuu
wa Serikali, Profesa Samwel Manyele alipokuwa akiongea na waandishi wa
habari mara baada ya kufungua mkutano wa wadau wa wakala wa afya ya
mazingira leo jijini Dar es Salaam.
“Kesi zinazopokelewa katika
maabara yetu zinazohusu sampuli ya Vinasaba kwa mwaka zinaonyesha kuwa
asilimia 49% kati ya asilimia 100% ya matokeo hayo huonyesha mzazi mmoja
ambaye ni baba kuwa si mzazi halali wa mtoto huyo”.
“Vinasaba ni utambulisho wa
kipekee wa kila kiumbe ambao unabeba taarifa muhimu na inayorithisha
tabia au umbile fulani la mhusika. Vinasaba ni kama vile kitabu cha
kumbukumbu kinachohusu maisha binafsi”, aliongeza Prof. Manyele.
Profesa Manyele aliongeza kuwa
mikoa ya kanda ya Ziwa, Arusha, Dar es Salaam na Mbeya ndio inayoongoza
kwa matokeo ya uchanguzi huo wa makosa ya Vinasaba nchini.
Akizungumza kuhusu lengo la
mkutano huo, Profesa Manyele amesema kuwa ni kuimarisha uhusiano uliopo
kati ya wadau wa kemikali na wadau wa afya ya mazingira kutoka katika
halmashauri tofauti nchini pamoja na ofisi ya Mazingira.
Aidha Profesa alibainisha
baadhi ya majukumu yanayofanywa na wakala wa Mkemia Mkuu wa Serikali
kuwa ni kufanya uchunguzi ili kuhakiki ubora na usalama wa vyakula,
dawa, maji, maji machafu, bidhaa za viwanda na mashambani, sampuli za
mazingira na sampuli zinazohusiana na makosa ya jinai.
“Matokeo ya uchunguzi wa makosa
ya jinai na vinasaba (DNA) huviwezesha vyombo husika kufikia maamuzi
stahili na kusaidia kutendeka kwa haki katika tuhuma za kesi za jinai
ikiwemo ulevi, mauaji, ubakaji, wizi wa watoto, uhalali wa mtoto kwa
mzazi, kwa kupitia vyombo husika” alifafanua Profesa.
Mbali na hayo, alisema wakala
kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto inatarajia kuwasilisha mapendekezo ya kutunga sheria ya kuunda
maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na Sheria ya kusimamia taaluma ya
Wakemia, kuimarisha upatikanaji wa mitambo na vifaa vya maabara kila
teknologia inapobadilika pamoja na kuimarisha zaidi taratibu za
uchunguzi ziwe za kisasa ili kuendana na mabadiliko ya sayansi na
teknologia
0 comments :
Post a Comment