Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akiwasili
katika Kiwanja cha Ndege cha Kigoma tayari kuanza ziara ya ukaguzi wa
miundombinu katika mikoa ya ukanda wa magharibi.
Meneja
wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), mkoa wa Kigoma, Eng. Narcis
Choma akitoa ufafanuzi kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Profesa Makame Mbarawa (aliyevaa kofia) kuhusu ujenzi wa barabara ya
Kidahwe-Kasulu Km 50 inayojengwa na China Railway 50 Group.
Ujenzi wa barabara ya Kidahwe-Kasulu Km 50 inayojengwa na Kampuni ya China Railway 50 Group ukiendelea.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (aliyevaa
kofia) akitoa maelekezo kwa wataalamu wa ujenzi wa kampuni ya China
Railway 50 Group baada ya kukagua mitambo yao ya kupima na kutafiti
udongo kabla ya kujenga barabara.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (aliyevaa
kofia) akitoa maelekezo kwa viongozi wa Wilaya ya Kasulu mara baaada ya
kukamatwa kwa vijana wawili (waliokaa chini) kutokana na wizi wa nyaya
za mkongo wa taifa, mkoani Kigoma.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (aliyevaa
koti la kaki) akiangalia athari za mmonyoko wa udongo zilizoathiri
mkongo wa taifa wa mawasiliano katika eneo la Kidahwe mkoani Kigoma.
……………………………………………………………..
Makandarasi wanaojenga barabara ya
Kidahwe-Kasulu Km 50 na Kibondo-Nyakanazi Km 50 wametakiwa kukamilisha
ujenzi huo mwezi Mei mwakani badala ya Novemba ili kuharakisha mkakati
wa Serikali wa kuufungua mkoa wa Kigoma kwa barabara za lami.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amesema hayo mara baada ya kukagua
ujenzi wa barabara hiyo uliyogawanywa sehemu mbili, Kidahwe-Kasulu
inayojengwa na China Railway 50 Group na Kibondo-Nyakanazi inayojengwa
na Nyanza Road Works.
Prof. Mbarawa amewataka
makandarasi hao kuongeza kasi ya ujenzi, vifaa na wafanyakazi wenye
sifa ili barabara hizo zikamilike kwa wakati na ubora unaotakiwa.
“Tutahakikisha ifikapo Juni mwaka
huu tutakuwa tumelipa madeni yote mnayoidai Serikali hivyo fanyeni kazi
kwa uhakika kwa kuwa katika kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Tano
tayari tumeshawalipa makandarasi zaidi ya shilingi bilioni 725”, amesema
Prof. Mbarawa.
Prof. Mbarawa amesisitiza kwamba
nia ya Serikali ni kuifungua mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi na Rukwa
kwa barabara za lami ili kufungua ukanda wa magharibi mwa nchi
kibiashara kutokana na ukanda huo kuwa sehemu muhimu ya nchi katika
uzalishaji na kiungo kikuu kwa nchi za Congo DRC, Burundi na Rwanda.
Katika hatua nyingine Waziri Prof.
Mbarawa amewataka wafanyakazi wa Shirika la Reli (TRL), kulinda
miundombinu ya reli na kujiepusha na vitendo vya hujuma ili kuliwezesha
shirika hilo kupata shehena kubwa ya mzigo kufuatia wadau mbalimbali
kuonesha nia ya kusafirisha mizigo kwa njia ya reli.
“Serikali imewekeza vya kutosha
katika Shirika la Reli hivyo mfanye kazi kibiashara ili mpate mzigo
mkubwa wa kusafirisha”, amesisitiza Prof. Mbarawa
Akizungumza na viongozi wa mkoa wa
Kigoma na taasisi zilizo chini ya wizara yake Prof. Mbarawa amewataka
kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuzuia uvamizi na uhujumu wa
miundombinu ya barabara, reli, na mkongo wa taifa wa mawasiliano na wote
watakaokiuka agizo hilo wachukuliwe hatua za haraka na za kisheria.
Prof. Mbarawa ametoa wiki moja kwa
taasisi zilizo chini ya wizara yake kuhakiki wafanyakazi ili kubaini
kama kuna wafanyakazi hewa.
Naye, Meneja wa Wakala wa Barabara
nchini (TANROADS), mkoa wa Kigoma, Eng. Narcis Choma amemhakikishia
Waziri Prof. Mbarawa kuwa mkoa wa Kigoma umejipanga vizuri katika
kudhibiti uvamizi wa miundombinu ya barabara na wale waliojenga ndani ya
mita 22 kwenye barabara kuu wataondolewa maramoja bila kulipwa fidia.
Prof. Mbarawa yuko katika ziara ya
kukagua miundombinu katika mikoa ya kanda ya magharibi ikiwa ni
utekelezaji wa mkakati wa Serikali wa uiboreshaji wa miundombinu ya
kanda hiyo ili kuiwezesha kufanya biashara kiurahisi na mikoa mingine ya
Tanzania na nchi za Congo DRC, Rwanda na Burundi.
0 comments :
Post a Comment