KATIBU MKUU KIONGOZI BALOZI OMBENI SEFUE |
1.0
Utangulizi
1.1
Jana, tarehe 30 Novemba, 2015, mahakama jijini
London ilitoza Standard Bank $ 32.2 milioni. Kati ya hizo $ 16.8 milioni ni
faini inayolipwa kwa Serious Fraud Office
(SFO), $8.4 milioni ni “disgorgement of
profits”; na $ 7 milioni zinalipwa kwa Serikali ya Tanzania. Fedha hizo ni
$ 6 milioni ambazo tulitozwa isivyostahili na $ 1 milioni ni riba ya fedha
hizo. Fedha tunazorejeshewa zililipwa isivyostahili kwa kampuni ya Kitanzania
iitwayo EGMA. Kesi inayohusika ilifunguliwa na SFO dhidi ya Standard Bank.
1.2
Mwaka 2012/13, Serikali ya Tanzania iliamua
kukopa fedha ($600 milioni) kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo. Huu ni
utaratibu wa kawaida, ambapo Serikali inaingia mkataba na Benki moja (Lead
arranger) ambayo inatafuta fedha kutoka kwenye benki na taasisi nyingine za
fedha. Ni utaratibu wa kawaida pia kuwa Lead
Arranger analipwa ada kwa kazi hiyo.
1.3
Serikali ya Tanzania ilitoa kazi hiyo kwa
Standard Bank, kupitia Stanbic (T) Ltd. Fedha tulizohitaji, $600 milioni ambazo
wakati huo zilikuwa sawa na Sh.947,673,240,000.00 zilipatikana na zikatumika
kama ilivyokusudiwa. Standard Bank ililipwa asilimia 2.4 ya fedha hizo kama ada
yao. Mkopo ulikuwa na masharti ya grace
period ya miaka miwili na nusu na kulipwa kwa miaka 7 (2019).
2.0
Uchunguzi
Nchini Tanzania
2.1
Mwaka 2013 kulikuwa na matatizo kwenye
Stanbic Bank (T) Ltd, wakati huo ikiongozwa na Bwana Bashir AWALE. Kwa kutumia
mamlaka yake chini ya Kifungu 47 cha Sheria ya Benki Kuu ya mwaka 2006 na
Kifungu 31 cha Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006, Benki Kuu
ilifanya ukaguzi wa kulenga (Targeted
Examination) benki hiyo.
2.2
Wakaguzi wa Benki Kuu, pamoja na mambo
mengine, walibaini malipo yasiyokuwa ya kawaida kuhusiana na kampuni ya Kitanzania
inayoitwa EGMA. Malipo hayo yalikuwa kinyume na taratibu za kibenki, na baadhi
ya watumishi wa Stanbic Bank (T) walishindwa kuvumilia hali hiyo. Wakaguzi wa
Benki Kuu walifuatilia malalamiko hayo na kujiridhisha kuwa uongozi wa Stanbic
Bank (T) ulifanya mambo ambayo ni kinyume na taratibu zinazokubalika kibenki.
Fedha kiasi cha $ 6 milioni kiliingizwa kwenye akaunti ya EGMA na siku chache
baadaye zilitolewa zote kwa fedha taslimu na wala benki haikukusanya kodi ya
zuio (withholding tax) kwa mujibu wa
sheria ya mapato ya kodi ya mwaka 2004 kutokana na mapato ya Standard Bank kwa
kazi ya ushauri iliyoifanya.
2.3
Kama ulivyo utaratibu, Benki Kuu ilitoa
taarifa ya ukaguzi kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Stanbic Bank (T) Ltd na kuitaka
Bodi hiyo kuchukua hatua za kurekebisha kasoro ndani ya benki, pamoja na kutoa
taarifa kwa Financial Intelligence Unit
kuhusiana na miamala yenye mashaka kwenye akaunti ya EGMA kwa mujibu wa Sheria
ya Anti-Money Laundering Act 2006.
2.4
Taarifa tulizopewa ni kuwa bodi ilikutana
na kuchukua hatua zinazostahili, ikiwemo kutoa taarifa FIU kuhusiana na miamala
kwenye akaunti ya EGMA, na kwa Wizara ya Fedha kuhusiana na kodi ya zuio.
2.5
Vile vile tumesikia kuwa bodi ya Standard
Bank iliona kuwa makosa yaliyobainishwa na wakaguzi wa Benki Kuu ya Tanzania
yalistahili kutolewa taarifa kwa SFO nchini Uingereza ambao walianzisha
uchunguzi ambao hatimaye ulipelekea kesi kufunguliwa.
3.0
Udanganyifu
ulivyofanyika
3.1
Kwa taarifa zilizopo, inaelekea kuwa
Standard Bank ilipanga kututoza ada ya asilimia 1.4 tu, yaani $ 8,400,000. Hata
hivyo ukafanyika ujanja wa kudai kuwa ati anahitajika local agent wa benki hiyo, ambaye naye alipwe asilimia 1 nyingine,
na kufikisha ada yote kuwa asilimia 2.4 ($14,400,000).
3.2
Local
agent huyo alikuwa kampuni ya EGMA, ambayo miamala yao
kuhusiana na hizo $6,000,000 walizochukua ndiyo ilishtua wakaguzi wa Benki Kuu
na taarifa kutolewa kwa Bodi ya Stanbic (T) Ltd na hatimaye Standard Bank, SFO
na Mahakama Uingereza.
4.0
Uchunguzi
Uingereza
4.1
Tarehe 29 Septemba, 2015, Mkuu wa Idara ya
Rushwa kwenye SFO aliiandikia Benki Kuu, akiomba ushirikiano wa Benki Kuu
kwenye uchunguzi na uendeshaji wa kesi dhidi ya Standard Bank Plc (ambayo sasa
inajulikana kama ICBC Standard Bank Plc).
4.2
Tarehe 29 Oktoba, 2015, Benki Kuu, iliiandikia
SFO kutoa taarifa kuhusu ukaguzi-lengwa ambao Benki Kuu iliufanya tarehe 15 –
19 Julai, 2013 kwenye Benki ya Stanbic Bank (T) Ltd. Ushahidi huo kutoka Benki
Kuu ulikuwa sehemu ya ushahidi uliosaidia SFO kushinda kesi. Katika kipindi
chote ambacho SFO ilikuwa inafanya uchunguzi, ilishirikiana na taasisi zetu
ikiwamo TAKUKURU, Benki Kuu, FIU na wengine. Mafanikio haya yaliyopelekea kwenye
uamuzi wa Tanzania kurejeshewa $ 7 milioni (Sh.15 bilioni/=) yametokana na
dhamira ya kweli ya Serikali ya Uingereza na Serikali ya Tanzania kupambana
na rushwa.
5.0
Hitimisho
5.1 Tunaishukuru
Serikali ya Uingereza, pamoja na SFO, kwa kuonesha njia katika kusaidia nchi
maskini zinazodhulumiwa na wapokea rushwa na watoa rushwa. Maana zipo nchi
nyingine tajiri ambazo wanapigia kelele rushwa kwa kuangalia upande wa mpokeaji
tu, na kusahau makampuni makubwa kutoka kwao yanayopenda kuhonga watu wetu.
Natoa wito kwa nchi nyingine tajiri kutoa ushirikiano kama huu wa Serikali ya
Uingereza. Nazishukuru taasisi zetu, Benki Kuu, na TAKUKURU, FIU na wengine kwa
kutimiza wajibu wao na kutoa ushirikiano kwa SFO uliowezesha SFO kushinda kesi
hii, na sisi kurejeshewa fedha ambazo zitatumika kutatua matatizo yetu ya
maendeleo na kero za wananchi.
5.2 Baada ya ushindi huo uchunguzi unaendelea ndani ya nchi ili tujue hizo $ 6 milioni zimekwenda wapi, na kama zilitumika kumhonga mtu tujue ni nani. Katika hili tutaomba ushirikiano wa wenye kampuni hiyo ya EGMA ambao kwa taarifa za vyombo vya habari vya Uingereza ni Bwana Harry KITILLYA, aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, Bwana MBOYA ambaye ni marehemu na Bwana Gasper NJUU.
0 comments :
Post a Comment